• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
DINI: Kukua si kuzeeka bali ni kubadilika kimaarifa, kimaadili na kisaikolojia

DINI: Kukua si kuzeeka bali ni kubadilika kimaarifa, kimaadili na kisaikolojia

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

KUKUA ni mtihani.

Kuzeeka si kukua.

Mtu anaweza kuwa mzee lakini anafanya ya kitoto, mpaka wanasema, fulani hakui.

Kuzeeka ni jambo la lazima lakini kukua ni chaguo lako.

Hapa tunazungumzia kukua kisaikolojia, kimaarifa, kiakili na kimaadili. Bwana wetu Yesu Kristo alikua kimaarifa.

Tunasoma hivi katika Biblia, “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake” (Luka2:40). Pia tunaambiwa, “Naye Yesu akazidi kukua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.” (Luka 2:52 ).

“Kama hatubadiliki hatukui. Kama hatukui hatuishi kweli,” alisema Gail Sheehy.

Tunakua kupitia uzoefu. Katika uzoefu kuna kujifunza kutokana na makosa.

“Watu wanakua kupitia uzoefu kama wanayakabili maisha kiukweli na kwa ujasiri. Tabia inajengwa namna hii,” alisema Eleanor Roosevelt.

Kukosa njia ni kujua njia. “Uzoefu ni jina ambalo watu huyapa makosa yao,” alisema Oscar Wilde.

Bill Gates anapenda kuwaajiri watu ambao wamefanya makosa, inaonyesha kuwa wanajiweka katika hatari.

Anasema, “Watu wanavyoshughulikia mambo yaliyokosewa ni ishara ya kushughulikia mabadiliko.”

Tunakua kupitia maumivu na mateso.

“Mtu hawezi kukua bila maumivu. Mtu hawezi kupiga hatua mbele bila maumivu. Mateso yanatuendesha kufanya mambo makubwa,” alisema Joe Abercromble.

Mbwa kama hajaungua mkia hatoki mekoni (Methali ya Tanzania).

Maumivu yanazaa jambo jema.

Mtalii wa kike aliitembelea Uswisi (Switzerland) na siku moja akafika kwenye malisho ya kondoo kilimani.

Alimwona mchungaji akiwa na kondoo wake wamepumzika kwa kumzunguka.

Karibu na rundo la nyasi alilala kondoo aliyeonekana kuwa na maumivu makubwa.

Mguu wake ulikuwa umevunjika. Mtalii aliuliza ilivyotokea.

Mchungaji alisema, “Nilivunja mguu wake. Kati ya kondoo wote katika kundi hili huyu ndiye alikuwa hatii hata kidogo; hakutii kamwe sauti yangu. Alitoroka na kutoa mfano mbaya kwa wengine. Nilivunja mguu wake kumsaidia na kuwasaidia wengine. Siku ya kwanza nilipomwendea na chakula alitaka kuning’ata. Nilimwacha siku kadhaa. Akapatwa na njaa. Nilirudi kwake kumpa chakula kwa sasa analamba mikono yangu. Kondoo huyu akipona atakuwa mfano mzuri wa kondoo kwenye kundi hili. Hakuna kondoo atakayesikia sauti yangu haraka sana kama kondoo huyu. Hakuna atakayenifuata upande mwangu kama kondoo huyu.”

Tunakua kwa kubadilika. Tunakuwa tunapotoka kwenye sanduku la mawazo mgando.

“Gharama ya kufanya kitu kilekile cha zamani ni kubwa zaidi ya gharama kubadilika,” alisema Bill Clinton. Kutobadilika kuna gharama kubwa sana. “Ni baada ya kutoka nje ya eneo la faraja, ndipo unaanza kubadilika, kukua na kubadilika,” alisema Roy T. Bennett.

Makinda wafundishwa kuruka

Mama mwewe huwafundisha makinda kuruka na kupaa kwa kufanya viota vyao visiwe eneo la faraja. Wanalazimishwa kutoka na kuruka. Kwa namna hiyo wanakua.

Tunakua kwa kuanguka. Nelson Mandela alithibitisha hilo aliposema, “Msinihukumu kwa mafanikio yangu, nihukumu kwa mara ngapi nilianguka na kuinuka tena.”

Unapoanguka na kuinuka unakua. Hata ng’ombe mwenye miguu mine uanguka. Tunakua kwa kushinda hofu.

“Mtu anaweza kuchagua kurudi nyuma kuelekea usalama au kwenda mbele kuelekea kukua. Kukua lazima kuchaguliwe tena na tena; lazima kuishinda hofu tena na tena,” alisema Abraham Maslow.

Tunakua kwa kuona mapya.

“Asemaye sijawahi kuona jambo hili, hajakua.”

Mtoto ambaye hatembei anafikiri mama yake ni mpishi mzuri sana (Methali ya Wahaya). Tembea uone. Tembea ukue. Jambo la msingi ni kujifunza mazuri na kuyafanyia kazi unapotembea.

Tunakua kupitia changamoto.

“Hatukui mambo yakiwa rahisi; tunakua tunapozikabili changamoto,” alisema Joyce Meyer.

Bahari shwari haitoi wanamaji stadi. Unapotaka kubadilika na kukua kuwa makini na watu unaoambatana nao.

Kadiri ya mwanasaikolojia wa kijamii Dr. David McCleland wa Havard, watu ambao unaambatana nao sana wanaitwa “kundi rejea” na hawa wanachangia asilimia 95 za mafanikio yako au kushindwa kwako.

You can share this post!

MWANASIASA NGANGARI: Mzungu wa kwanza kuwa waziri baada ya...

Ruto kukosa nyama-choma Amerika

adminleo