• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Raila anavyomuandaa bintiye Winnie kumrithi kisiasa

Raila anavyomuandaa bintiye Winnie kumrithi kisiasa

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kinara wa NASA, Raila Odinga kuandamana na bintiye Winnie ‘Kazi’ Odinga alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Ijumaa imeangaziwa na wachanganuzi kama ishara kuwa kigogo huyo wa upinzani anamuandaa kumrithi atakapostaafu siasa.

KULINGANA na wachanganuzi wa siasa, familia ya Jaramogi Oginga Odinga imewekeza sana katika siasa na ni azma ya Bw Odinga kuhakikisha himaya hiyo inaendelea kuimarika chini ya mmoja wa wanawe atakapostaafu.

Hii ndiyo sababu iliyomfanya kuandamana naye Harambee House kukutana na Rais Kenyatta kama njia ya kumpa uzoefu wa siasa za kitaifa.

Bw Odinga ana umri wa miaka 73 na muda wake kuendelea kucheza siasa kali unayoyoma. Ndiposa anaweka mikakati ya atakayechukua hatamu kutoka kwake atakapoamua kupumzika.

Wakati mmoja Winnie aliambia runinga kuwa babake alianza kumhusisha katika siasa akiwa na umri wa miaka sita pekee, ikionekana kama hatua ya kuweka msingi wake kwenye siasa.

Mpango wa Bw Odinga kumkabidhi bintiye usukani unajitokeza wazi ikingatiwa kuwa aliamua kufichua siri ya kikao hicho kwa bintinye huku akiwaacha vinara wenzake katika NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula gizani.

Wengi walitarajia kuwa Bw Odinga angempokeza mmoja kati ya vinara hao uongozi lakini hatua ya kuwapuuza inaonyesha hawamo kwenye hesabu yake.

Picha ya ‘selfie’ ya Raila Odinga na bintiye Winnie ‘Kazi’ Odinga wakiwa kwa gari. Picha/ Hisani

Mwandani

Akiwa kitinda mimba wa Bw Odinga, Winnie, aliye na umri wa miaka 28, amekuwa mwandani wa baba yake na alisimamia ofisi ya kampeni zake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Pia alikuwa akimhusisha katika maamuzi ya kisiasa.

Winnie, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya biashara na mawasiliano amekuwa akiandamana na baba yake kwenye hafla tofauti za kisiasa nchini na ng’ambo na hata kushiriki maandamano yaliyoitishwa na muungano wa NASA.

Mnamo Disemba 17 mwaka jana, aliwasili nchini pamoja na baba yake kutoka Amerika, umati wa wafuasi wa NASA ulipomlaki katika uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta na vurugu zikazuka polisi wakikabiliana na waandamanaji.

 

Rais wa kwanza mwanamke

Wiki iliyopita, mdadisi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi alishangaza wafuasi wake mtandaoni alipodai kwamba Winnie ndiye atakayekuwa rais wa kwanza kutoka jamii ya Waluo na wa kwanza mwanamke wa Kenya.

“Wamesema kwamba ingawa nyota yake ya kisiasa ya Raila imezima, bado kuna matumaini kwamba binti yake Winnie Odinga atakuwa rais wa kwanza mwanamke wa Kenya,” Bw Ngunyi ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Bw Odinga alisema.

Alisema kwamba Raila ni mwanasiasa mwerevu na mjanja ambaye alianza kupanga na kumuandaa mrithi wake mapema.

Akihojiwa na gazeti moja awali, Winnie alijifananisha na mlinzi, msaidizi na dereva wa baba yake kuashiria uhusiano wao wa karibu.

 

 

 

 

You can share this post!

Moi asafirishwa Israeli kwa matibabu ya dharura

Klabu zilizopandishwa zakosa ustadi unaohitajika ligi ya...

adminleo