• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Mwanamuziki aliyeikejeli jamii ya Wakamba motoni

Mwanamuziki aliyeikejeli jamii ya Wakamba motoni

John Gichiri Njau akiwa katika mahakama ya Nairobi Machi 12, 2018 alikoshtakiwa kwa makosa 3 ya uchochezi dhidi ya jamii ya Wakamba kupitia kwa muziki wake. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh700,000. Kesi kusikizwa Aprili 11. Picha/Paul Waweru

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMUZIKI ambaye wimbo aliotunga wa kuikejeli jamii ya Wakamba alishtakiwa jana kwa uchochezi. Wimbo huo ulikuwa umetungwa na kuimbwa kwa lugha ya Gikuyu.

Kabla ya kukamatwa na kufikishwa kortini viongozi mbali mbali wakiongozwa na Seneta Mutula Kilonzo waliandika barua ya malalamiko na kutoa wito Bw John Gichiri Njau akamatwe na kushtakiwa.

Alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi , Bw Francis Andayi, Bw Njau alikanusha mashtaka matatu ya kueneza chuki na uchochezi wa kikabila.

Bw Andayi alielezwa kwamba muziki huo alioporomosha Bw Njau ulilenga kueneza chuki na kuzua cheche za kikabila dhidi ya Jamii za Agikuyu na Wakamba.

“Muziki aliotunga na kuimba ulisambazwa katika mitandao ya kijamii,” Bw Andayi alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha.

Bw Andayi alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha kwamba, Bw Njau alitunga nyimbo kwa lugha ya Gikuyu za kuzua chuki na uchochezi baina ya kabila la Wakamba na Wagikuyu kuhusu uchomaji makaa na ulaji maembe, ndege wa angani na hata mbwa kutokana na dhiki ya njaa.

Bw Naulikha alimweleza hakimu kwamba nyimbo hizo zilizoimbwa kwa lugha ya Gikuyu na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza zilikuwa zinaishushia hadhi jamii ya Wakamba.

Kanda ya muziki huu inazugumzia biashara ya makaa ambayo imepigwa marufuku katika mojawapo ya kaunti 47.

Gavana wa Kitui Charity Ngilu alipiga marufuku uchomaji makaa na usombaji wa changarawe.

“Wimbo huu umetafsiriwa kama ulivyo nakiliwa kwa hati ya mashtaka,” alisema Bw Naulikha.

Katika shtaka la kwanza Bw Njau ameshtakiwa kuimba anadai jamii ya Wakamba itaanza kula ndege na kwamba imelaaniwa. Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Bw Naulikha hakupinga ombi hilo ila aliomba mahakama itilie maanani uzito wa maneno anayodaiwa alisema Bw Njau.

Korti ilielezwa adhabu itakayopitishwa dhidi ya Bw Njau ni kali.

Bw Andayi alimwachilia kwa dhamana ya Sh700,000 pesa taslimu na kuorodhesha kesi hiyo isikizwe Aprili 11, 2018.

 

You can share this post!

Zambia kuwasukuma jela watakaonaswa wakiwa na...

Raila awekwa kwenye mkeka na vinara wenza

adminleo