• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Raila awekwa kwenye mkeka na vinara wenza

Raila awekwa kwenye mkeka na vinara wenza

Na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Bw Odinga aliwashtua wenzake Ijumaa alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta bila kuwajulisha, jambo ambalo lilionekana kuwakera
  • Vinara wenza walimsikiliza, wakauliza maswali, akajibu na kuwaeleza kinaganaga waliyozungumza na Uhuru
  • Licha ya vinara hao kukutana na kujaribu kuonyesha hadharani kuwa bado muungano uko imara,  Bw Mudavadi alikiri ni “zito mno”
  • Vinara hao watahitaji kukutana tena siku zijazo kabla watangaze msimamo wao wa mwisho kama muungano

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, Jumatatu aliwekwa kwenye kiti moto na vinara wenzake wa Muungano wa NASA kwa zaidi ya saa wakitaka awaeleze kuhusu sababu za kuwaacha gizani alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta, Ijumaa iliyopita na ni masuala gani waliyojadiliana.

Katika mkutano wa kitengo kikuu zaidi cha NASA ambacho wanachama wake ni Bw Odinga na vinara wenzake Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Musalia Mudavadi (Amani National Congress), kigogo huyo alitakiwa kueleza kwa nini alichukua hatua iliyoonekana kusaliti mkataba wa NASA.

“Leo tumepata nafasi ya kumsikiliza Mheshimiwa Raila Odinga kuhusu majadiiliano waliyofanya na Uhuru Kenyatta Ijumaa iliyopita.

Tumesikiliza aliyotueleza, tumeuliza maswali, amejibu na ametueleza kinaganaga waliyozungumza,” akasema Bw Mudavadi baada ya mkutano huo uliofanywa katika Hoteli ya Stoni Athi, Kaunti ya Machakos.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wanachama wa kamati ya usimamizi wa NASA wakiwemo Seneta wa Siaya James Orengo, aliyekuwa Seneta wa Machakos Bw Johnstone Muthama, na wabunge Eseli Simiyu (Tongaren), na Sakwa Bunyasi (Nambale).

Bw Odinga aliwashtua wenzake Ijumaa alipokutana na Rais Uhuru Kenyatta bila kuwajulisha, jambo ambalo lilionekana kuwakera. Ndiposa jana walimweka kinara wao kwenye mkeka kutaka kufahamu sababu za kuwaweka gizani na ni yapi walijadiliana na Rais Kenyatta.

Vinara wa NASA pamoja na wanachama wa kamati ya usimamizi ya muungano huo walipokutana na Bw Odinga kuhusu hatua yake ya kuungana na Rais Kenyatta katika Hoteli ya Stoni Athi, Kaunti ya Machakos Machi 12, 2018. Picha/MAKTABA

Ingawa Bw Mudavadi hakufichua masuala halisi waliyogusia walipomhoji Bw Odinga, ilibainika alifanikiwa kuwashawishi kwamba maelewano kati yake na rais hayataathiri juhudi zilizokuwa zimeanzishwa na upinzani kupigania mabadiliko nchini.

Muungano huo umekuwa ukiitisha mdahalo wa kitaifa kujadili jinsi ya kutatua changamoto zinazokumba taifa kwa masuala kama vile uhuru wa mahakama, mfumo wa uchaguzi wenye haki, jinsi ya kukabiliana na umaskini na kuleta usawa baina ya wananchi bila kujali kabila wala vyama wanavyounga mkono.

Masuala kadhaa kati ya hayo yalikuwa kwenye maelewano ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, ingawa haikuwa wazi jinsi yatakavyosuluhishwa kwani walichagua Mabw Paul Mwangi na Martin Kimani mtawalia kuongoza utekelezaji wa makubaliano yao.

Baadhi ya viongozi wa upinzani hawakufurahishwa na hatua hiyo kwa kuwa haikuhusisha msimamo wa vyama vyote tanzu.

 

‘Tuko tayari’

“Tunashukuru kuwa sasa mlango umefunguliwa kwa mashauriano. Msimamo wetu kama NASA ni kuwa tuko tayari kwa mashauriano hata sasa kwa sababu tunataka majadiliano ya kikweli ambayo yatasuluhisha mambo tunayojua ni mazito katika taifa letu,” akasema Bw Mudavadi.

Licha ya vinara hao kukutana na kujaribu kuonyesha hadharani kuwa bado muungano uko imara, ilionekana suala hilo ambalo Bw Mudavadi alikiri ni “zito mno” halijafikia kikomo.

Vinara wote watahitajika kwenda kuarifu maafisa wakuu wa vyama vyao kuhusu yaliyojiri, na uamuzi wa mwisho utaachwa mikononi mwa wanachama kuamua kama wataunga mkono mwelekeo uliochukuliwa na Bw Odinga au la.

Zaidi ya hayo, vinara hao watahitaji kukutana tena siku zijazo kabla watangaze msimamo wao wa mwisho kama muungano.

Bw Wetang’ula na Bw Musyoka walikuwa wamekutana usiku wa kuamkia jana ingawa haikubainika wazi yale waliyojadili kwenye mkutano wao wa faraghani.

 

You can share this post!

Mwanamuziki aliyeikejeli jamii ya Wakamba motoni

Majaji waliosikiliza kesi ya Ruto ICC wapandishwa vyeo

adminleo