• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Wamalwa mbioni kubadilisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu

Wamalwa mbioni kubadilisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu

Na CHARLES WASONGA 

MSWADA wa kubadilisha tarehe ya Uchaguzi Mkuu kutoka Agosti 8 hadi  Desemba uliwasilishwa bungeni Jumatano.

Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa ndiye mdhamini wa mswada huo ambao utalenga kubadili tarehe ya uchaguzi kutoka Agosti 8, 2018 mwaka wa tano baada ya uchaguzi hadi Jumatatu ya tatu mwezi Desemba mwaka huo.

Bw Wamalwa ambaye ni naibu kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa alisema shughuli hiyo ikifanyika Agosti huhitilafiana na kalenda ya elimu na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa.

Hii ni endapo kutatokea haja ya kuandaliwa kwa awamu ya pili ya uchaguzi wa urais au endapo matokeo yake yatabatilishwa na mahakama ya juu jinsi ilivyofanyika Septemba 1, mwaka 2017.

“Lengo la mswada huu ni kuifanyia mabadiliko vipengee vya 101 (1), 136 (2) (a), 177 (a) na 180 (1) vya Katiba ya Kenya ili kubadilisha tarehe ya sasa ya uchaguzi mkuu wa wabunge, urais, madiwani, magavana na manaibu wao kutoka Jumanne mwezi Agosti ya kila mwaka wa tano hadi Desemba kila mwaka wa tano,” mswada huo unasema.

 

Utalii

“Marekebisho haya ya Katiba yanalenga kuhakikisha kuwa joto la uchaguzi haliathiri kunawiri kwa msimu wa watalii wengi kutembelea Kenya ambao huwa ni Agosti kila mwaka. Huo ni wakati ambapo Wakenya wengi huwa hawana haja ya kuacha shughuli zao muhimu kushiriki uchaguzi,” mswada huo unaongeza.

Mwaka 2017, kipindi cha uchaguzi kiliongezeka baada ya mahakama ya juu kubatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta na kuamuru marudio ya uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 26, 2018. Hatua hiyo iliilazimu Wizara ya Elimu kusongeza mbele tarehe ya  kufanywa kwa mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne (KCSE) na ile ya kitaifa ya darasa la nane (KCPE) ili wanafunzi wasisumbuliwe na zoezi hilo la marudio ya uchaguzi.

KCSE iliendeshwa  kuanzia Oktoba 6 huku KCPE ikianza Oktoba 30 na kukamilika Novemba 2.

Hii sio mara ya kwanza wabunge kujaribu kubadilisha tarehe ya uchaguzi kupitia mswada. Jaribio sawa na hili la Bw Wamalwa lilifanywa na aliyekuwa Mbunge wa Ugenya David Ochieng lakini likafeli baada ya kukosa kupata uungwaji mkono wa thuluthi mbili ya wabunge wote 349, ambayo ni wabunge 233.

Kwa hivyo, Mbunge huyo wa Kiminini atalazimika kusaka uungwaji mkono kutoka kwa wabunge 233 ili kabla ya kutiwa saini kuwa sheria.

You can share this post!

Hakuna nusu mkate, Duale afafanua

KAULI YA WALIBORA: Dhana kwamba ufahamu wa lugha aghalabu...

adminleo