• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Mashemeji wamtaka alipe mahari kwa kurithi mke baada ya mume kuaga

Mashemeji wamtaka alipe mahari kwa kurithi mke baada ya mume kuaga

Na TOBBIE WEKESA

AHERO, KISUMU

MAKALAMENI kutoka hapa waliwashangaza wakazi walipomdai polo mahari kwa kumrithi dada yao baada ya mumewe kufariki.

Inasemekana makalameni hao walimlazimisha polo kuwapa ng’ombe watatu ili kukamilisha deni alilokuwa ameacha marehemu mume wa dada yao.

Mume wa kipusa aliaga dunia miaka miwili iliyopita. Jamaa kutoka kwa familia ya marehemu alijitokeza na kumrithi mjane. Duru zinasema kabla ya marehemu kuaga dunia, alikuwa amepeleka ng’ombe wawili kama mahari na kuahidi kupeleka ng’ombe wengine wawili baada ya miaka miwili.

“Tunachojua marehemu shemeji yetu alikuwa amempa mama kitu kidogo na akaahidi kumalizia baadaye. Ni wewe utamalizia,” kalameni mmoja alimueleza polo.

Polo alijaribu kupinga madai ya makalameni lakini juhudi zake hazikufua dafu. “Unatuambia nini? Hata kuna fununu kwamba dada yetu ana mimba yako. Hatutoki hapa bila mahari,” makalameni waliapa.

Polo aliwaeleza makalameni kwamba alikuwa akimsaidia mjane ili asitaabike bali hakuwa amemrithi.

“Acha zako. Hadithi zote twazijua. Umemrithi tangu shemeji aage dunia. Kwa sasa tunachukulia kuwa umemuoa,” makalameni walimueleza polo.

Inadaiwa polo aliamua kuwaita wazee wa jamii ili kutatua mgogoro uliokuwa ukinukia.

Wazee walijaribu kutuliza joto lakini makalameni walisisitiza lazima polo atoe mahari.

“Kwanza huyu jamaa tumemsamehe sana. Angeanza kulipa mahari freshi. Kama hatatoa mahari anataka tumtambue kama nani? Hakuna vya bure. Lazima mahari atoe na ni leo,” makalameni walisisitiza.

Wazee walilazimika kuondoka na kumuacha polo ang’ang’ane na wageni wake.

…WAZO BONZO…
…WAZO BONZO…

You can share this post!

Koros ashuku alitolewa kafara

DOMO KAYA: Muacheni Bahati na ya kwake, hayawahusu ndewe...

adminleo