• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 10:55 AM
Bodi ya KNH imeshindwa na kazi, nyingine iundwe, kamati yapendekeza

Bodi ya KNH imeshindwa na kazi, nyingine iundwe, kamati yapendekeza

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, Bi Sabina Chege. Picha/ Maktaba

Na LUCY KILALO

KAMATI ya Afya ya Bunge la Kitaifa imependekeza kuundwa kwa Bodi mpya ya Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) ikisema kuwa iliyopo sasa imeshindwa kutekeleza majukumu yake.

Mapendekezo hayo yametolewa kwenye ripoti iliyowasilishwa Jumanne bungeni na mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi Sabina Chege.

Ripoti hiyo ilikuwa kuhusu uchunguzi wa madai ya ubakaji katika hospitali hiyo, upasuaji uliofanywa kwa mgonjwa ambaye hakustahili, wizi wa mtoto, kudorora kwa vifaa vya matibabu miongoni mwa hali nyingine za jinsi shughuli zinavyoendeshwa hospitalini humo.

“Kwa kutambua kuwa Bodi imeshindwa kutekeleza majukumu yake kulingana na matakwa ya kitaifa, mwenye mamlaka ya kuteua kulingana na Sehemu ya 7(3) ya Sheria ya Mashirika ya Serikali, Kitengo cha 446, aunde Bodi mpya,” ripoti hiyo imependekeza.

Inaongeza: “Bodi mpya iangalie wasimamizi wa ngazi za juu kwa lengo la kuweka mfanyakazi anayestahili na wenye sifa zinazostahili katika nafasi hizo.”

Wakati huo huo, kamati hiyo imesema kuwa haikupata ushahidi kuweza kufafanua madai ya dhuluma za kingono hospitalini humo. Hata hivyo, imetaka kitengo cha upelelezi kikamilishe uchunguzi wake kuhusiana na madai ya ubakaji na kuwasilisha ripoti yake katika muda wa siku 14.

Pia idara hiyo inahitajika kuwasilisha ripoti kuhusiana na mgonjwa ambaye aliuawa kwa kudungwa kisu miaka michache iliyopita.

Kamati hiyo pia inataka utaratibu unaotumiwa kuelekeza wagonjwa kwa hospitali za rufaa uzingatiwe, pamoja na kuyataka mashirika yanayodumisha viwango kuhakikisha utaalamu unadumishwa katika sekta ya afya.

Vile vile, imekiri kuwa utekelezaji wa mifumo inayostahili hauzingatiwi, vifaa vilivyopo vimepitwa na wakati, kuna upungufu wa wahudumu wa matibabu, upungufu katika uongozi, msongamano, na kukosa ufadhili wa kutosha kutoka kwa serikali kuwa baadhi ya hali zinazochangia masaibu yanayoshuhudiwa Kenyatta, hasa tukio la makosa ya upasuaji.

Hospitali ya Kenyatta ndiyo kubwa zaidi nchini na kulingana na mpangilio inafaa kupokea wagonjwa wanaotumwa kwa matibabu maalum kutoka hospitali zingine.

Lakini hali ilivyo sasa inapokea wagonjwa wanaozuru huko moja kwa moja bila ushauri wa hospitali zingine, hali inayosababisha msongamano mkubwa.

 

You can share this post!

Ajuta kukopa Sh700,000 kutoka kwa benki kulipa mganga

Kifaru mweupe wa mwisho duniani aaga kwa kuzeeka

adminleo