• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Wazito FC wamridhisha kocha kwa bidii yao

Wazito FC wamridhisha kocha kwa bidii yao

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa Klabu ya Wazito FC Francis Ouna amesifu juhudi zinazotiwa na kikosi chake katika kubadilisha mwanzo mbaya wa msimu baada ya timu hiyo kusajili ushindi wa pili kwenye ligi kuu ya KPL.

Akizungumzia matokeo ya wikendi ambapo Wazito waliwaaibisha Nakumatt FC kwa kichapo cha 2-0 uwanjani Camp Toyoyo, mkufunzi huyo alisema bidii wanayotia mazoezini hatimaye imeanza kuwazalishia matunda.

“Tunafanya mazoezi ya uhakika na tulicheza vizuri tukijua ushindi huo ungetuvusha mbele ya wapinzani waliokuwa mbele yetu kwenye msimamo wa jedwali kwa alama moja tu,” akasisitiza kocha Ouna.

Wazito FC ambao walipandishwa kushiriki KPL mwisho wa msimu uliopita wamekuwa na mwanzo wa wastani tangu msimu uanze wakipoteza mechi mbili, kushinda mbili na kubwagwa mara tatu.

Walibwagwa na timu za Kariobangi Sharks, AFC Leopards na Bandari huku wakienda sare dhidi ya klabu za Kakamega Homeboyz na Posta Rangers.

Kabla ya kuifunga Nakumatt  ambao pia walipandishwa ligini, walikuwa wamesajili ushindi mmoja pekee dhidi ya wanasukari Sony Sugar.

Kwa sasa Wazito wanashikilia nafasi ya kumi kwenye msimamo wa jedwali la ligi na wana matumaini makubwa ya kupata ushindi watakapochuana na klabu ya Zoo Kericho Jumatano ijayo Kericho Green Stadium.

Wikendi hii mechi za ligi hazitasakatwa ili kupisha michuano ya kimataifa. Baadhi ya wachezaji wanaowajibikia klabu za hapa nchini wanatarajiwa kuchezea timu ya taifa Harambee Stars dhidi ya Comoros siku ya Jumamosi.

You can share this post!

Kocha wa Vihiga United aomba radhi kwa kuropokwa uwanjani

Aibu kwa viongozi wa Laikipia wanafunzi kutumia mawe kama...

adminleo