• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Okumbi apigwa kalamu kwa matokeo duni ya Harambee Stars

Okumbi apigwa kalamu kwa matokeo duni ya Harambee Stars

Na JOHN ASHIHUNDU

KOCHA wa Harambee Stars, Stanley Okumbi amefutwa kazi Jumatano pamoja na wasaidizi wake, Frank Ouna na Haggai Azande.

Watatu hao ametimuliwa mfupi tu baada ya timu hiyo ya taifa kuchapwa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CRA) katika mechi ya kupimana nguvu nchini Morocco mapema juma hili.

Matokeo hayo yalifuatia sare ya 2-2 ya mwishoni mwa wiki dhidi ya limbukeni Comoros katika mechi nyingine ya kirafiki, pia nchini humo.

Comoros ambao wako nyuma ya Kenya mara 27 katika viwango vya kimataifa vya FIFA, wanashikilia nafasi ya 132 kwenye orodha hiyo ya Dunia.

Okumbi amekuwa akishikilia uadhifa huo kwa muda baada ya Paul Put kujiuzulu Februari.

Taarifa kutoka FKF ilisema Ukumbi amepewa jukumu la kuinoa timu ya vijana wasiozidi umri wa miaka 20 inayojiandaa kushiriki mechi za vijana za mchujo wa kufuzu kwa fainali za AFCON.

Hii ni mara ya pili kwa Okumbi kupewa jukumu la kuwa kocha mkuu wa Harambee Stars baada ya hapo awali kupewa kazi hiyo mwezi Februari 2016 na kuhudumu hadi Novemba 2017 baada ya Bobby Williamson kung’atuka. Alishushwa na kuwa naibu wa Put aliyeajiriwa Februari 2018.

Haikujulikana haraka majukumu watakayopewa Ouna na Azande, lakini wataendelea kufanya kazi katika klabu za Wazito FC na Tusker mtawaliwa.

Katika mechi yao ya Jumanne, CAR walipata mabao ya ushindi kupitia kwa Foxi Kethevomano, Dagalou Eudes na Moimi Hilare, huku ya Stars ikijibu kupitia kwa Erick Johana na Michael Olunga.

Juhudi za Okumbi kuwaingiza Paul Were na Timbe katika nafasi za Clifton Miheso na Jesse Were kwa ajili ya kupata mabao ziliambulia patupu.

Ismail Gonzalez wa Stars alionyeshwa kadi nyekundu na kutolewa nje katika mechi hiyo iliyochezewa mjini Marakech.

Dhidi ya Comoros, Stars ilijipatia mabao yake kupitia kwa kiungo wa Tottenham Hotspur, Victor Wanyama na winga wa Buildcon nchini Zambia, Miheso.

Wanyama alifunga penalti baada ya Eric Johanna wa IF Brommapojkarna ya Uswidi kuangushwa ndani ya kijisanduku na beki, Chaker Alhdhur.

You can share this post!

Mtoto aliyejitwika jukumu la kumlea mamaye mlemavu

Matokeo mseto kwa klabu za Kenya voliboli Misri

adminleo