• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kesi ya Miguna: Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa kujua hatima yao Alhamisi

Kesi ya Miguna: Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa kujua hatima yao Alhamisi

Na RICHARD MUNGUTI

Kwa ufupi:

  • Jaji George Odunga awapata na hatia Mabw Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet ya kudharau na kukaidi maagizo ya mahakama kwa kukataa kumwachilia huru Dkt Miguna
  • Vitendo vya baadhi ya mawaziri na wakuu serikalini, ni ithibati wazi kuwa wanaendelea kuishi katika enzi ya zamani ambapo haki za wananchi zinahujumiwa kiholela, asema jaji huyo 
  • Jaji Odunga aamuru Dkt Miguna aachiliwe mara moja na ikiwa maafisa wa Uhamiaji na Mkuu wa Polisi JKIA hawatamwachilia, Mabw Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet hawatasikizwa wakifika kortini Alhamisi
  • Masaibu ya Miguna yalianza alipomwapisha kinara wa Nasa Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018, lakini tamati ya kizugumkuti hiki ni Alhamisi

MBIVU na mbichi zitajulikana Alhamisi wakati Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i , Inspekta Jenerali wa  Polisi (IG) Joseph Boinnet  na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Meja Mstaafu Gordon Kihalangwa watafika katika Mahakama Kuu kuhukumiwa kwa kukaidi agizo la kumwachilia huru wakili mbishi Dkt Miguna Miguna ambaye amezuiliwa ndani ya choo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa muda wa saa 72 sasa.

Watatu hao wamepatikana na hatia ya kukaidi agizo wamachilie Dkt Miguna na huenda wakawa maafisa wakuu katika serikali ya Jubilee kusukumwa jela.

Uamuzi dhidi yao utakaotolewa Alhamisi utakuwa wa kihistoria kwa vile mahakama inatarajiwa kudhihirisha uwezo wa mamlaka yake.

Mahakama pia inatazamiwa kuamuru kwamba watatu hao pamoja na mwanasheria mkuu ambaye ni mshauri mkuu wa Serikali “hawafai kuhudumu katika nyadhifa za umma.”

Wakisukumwa jela watapoteza nyadhifa wanazoshikilia na siku za usoni hawatakubaliwa kuhudumu kwa vile wamekaidi vifungu nambari 10 na 6 vya sheria. Vyote vinazugumzia maadili ya wanaohudumu katika nyadhifa za umma.

Macho yote yanamtazama Jaji George Odunga ambaye aliwapata na hatia Mabw Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet ya kudharau na kukaidi maagizo ya mahakama kwa kukataa kumwachilia Miguna hapo Jumatano.

Mawakili wa Dkt Miguna Dkt John Khaminwa, Lawrence Sifuna, James Orengo, Nelson Havi na Otiende Amolo wakiwa katika Mahakama Kuu Machi 28, 2018 jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Ndani miezi 6

Jaji Odunga aliombwa awasukume jela miezi sita kila mmoja na kuwaamuru walipe faini ya Sh200,000 kutoka kwa mifuko yao.

Alipowapata na hatia, Jaji Odunga alisema watatu hao walidharau korti na maagizo iliyotoa na badala ya kuonyesha heshima kufika kortini Jumatano alasiri wakiandamana na Dkt Miguna walihepa wakidai walikuwa wanahudhuria gwaride la kufuzu kwa maafisa wa kikosi cha polisi cha GSU mtaani Embakasi, Nairobi.

“Badala ya kufika kortini, watatu hao walitoroka na kukataa katakata kumwachilia Dkt Miguna. Haya ni madharau dhidi ya mamlaka ya mahakama,” akasema Jaji Odunga.

Jaji huyo alisema ni jambo la kusikitisha kabisa kwa vile “baadhi ya mawaziri wanajichukua kwamba wao ndio sheria na hawana haja ya kutii sheria na maagizo ya mahakama.”

Alisema kwamba ni masikitiko makubwa kwa vile baadhi ya mawaziri na wakuu serikalini hawajatambua katiba iliyopitishwa Agosti 27, 2010 na umuhimu wake.

Jaji huyo alisema kutokana na vitendo vya baadhi ya mawaziri na wakuu serikalini, ni wazi wanaendelea kuishi katika enzi ya zamani ambapo haki za wananchi zinahujumiwa kiholela.

Akizungumzia juu ya kesi ya Dkt Miguna, Jaji Odunga alisema aliwaamuru Dkt Matiang’i, Bw Boinnet na Bw Kihalangwa kufika mbele  yake Jumatano saa nane “kuadhibiwa kwa kudharau maagizo ya mahakama.”

Mawakili wa KNHRC Judy Lema na Victor Kamau wakiwa kortini Machi 28, 2018 katika kesi ya Dkt Miguna Miguna jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Miguna aachiliwe mara moja

Na wakati huo huo Jaji Odunga aliamuru Dkt Miguna aachiliwe mara moja na ikiwa “maafisa wa Uhamiaji na Mkuu wa Polisi JKIA hawatamwachilia, Mabw Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet hawatasikizwa wakifika kortini Alhamisi.”

Vile vile jaji huyo aliamuru walinzi katika JKIA wawaruhusu Mawakili Dkt John Khaminwa , James Orengo, Otiende Amolo, Cliff Ombeta , Harun Ndubi na Aulo Soweto wamwone Dkt Miguna pasi kuweka vikwazo vyovyote.

“Naamuru kwamba Dkt Miguna asalie humu nchini na wala asisafirishwe kama alivyofanyiwa Feburuari 9, 2018 akitarajiwa kortini,” alisema Jaji Odunga.

Alisema watatu hao waliagizwa wamwachilie Dkt Miguna Jumanne na badala yake wakamzuilia kinyume cha maagizo ya  Jaji Roselyn Aburili. Jaji huyo alikuwa amesema Dkt Miguna aachiliwe huru bila masharti.

Pia jaji huyo alikuwa ameagiza Dkt Miguna afike kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi aliyowashtaki watatu hao kwa kuvunja haki zake.

Mawakili wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNHRC) waliunga mkono ombi Dkt Matiang’i, Kihalangwa na Boinnet wasUkumwe jela miezi sita na watozwe faini watakayolipa wenyewe na isigharamiwe na pesa za umma,

“Bali na faini hiyo na adhabu hiyo, naomba hii mahakama iamuru watatu hao wasihudumu katika nyadhifa za umma ama hata kushika milango ya afisi za umma,” akasema wakili Victor Kamau wa KNHRC.

Mawakili wa Dkt Miguna Dkt John Khaminwa, Lawrence Sifuna, James Orengo, Nelson Havi na Otiende Amolo wanywa kahawa baada ya siku ndefu mahakamani Machi 28, 2018 jijini Nairobi. Picha/ Richard Munguti

Mateso ya Miguna

Bw Kamau alisema wakili  Miguna aliteswa na kuraruriwa nguo na kusukumwa ndani ya Ndege kupelekwa Dubai kinyume cha sheria huku haki zake za kuwa nchini bila cheti cha kusafiria na hata nguo ama hati zozote zikihujumiwa.

“Huu ni ukiukaji wa hali ya juu wa haki za binadamu,” alisema Bw Kamau.

Mahakama ilisema watatu hao walikaidi maagizo ya Majaji Luka Kimaru na Enock Mwita kwamba hawapasi kumtangaza Dkt Miguna mwananchi haramu.

Badala ya kumfikisha kortini kama walivyoagizwa na Jaji Kimaru, idara ya uhamiaji ilimsomba na kumsafirisha hadi nchini Canada.

Mawakili walisema walipoteza zaidi ya saa 320 wakifanya kesi hiyo na maagizo waliypopata yakapuuzwa na kudharualiwa.

Mwanaharakati Okiya Omtatah alikuwa miongoni mwa waliohudhuria kesi ya Miguna Miguna mbele ya Jaji George Odunga Machi 28, 2018. Picha/ Richard Munguti

“Kesi hii sasa ni ile ya kudharau korti yenyewe,” alisema Jaji Odunga na kuongeza lazima “sheria ifuatwe na kila mtu kwa vile hakuna mmoja aliye mkuu kuliko sheria na hakuna aliye juu ya sheria.

Masaibu ya Miguna yalianza alipomwapisha kinara wa Nasa Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018.

Polisi walivunja makazi yake na kumkamata kisha wakamzuilia kwa siku mbili ndipo Jaji Luka Kimaru akaamuru afikishwe kortini.

Jaji Kimaru alikaa kortini hadi saa mbili kasorobo ila Miguna hakuletwa licha ya hakikisho ya kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu.

Usiku huo wa Feburuari 9, 2018 Miguna alifurushwa na kupelekwa Canada na idara ya Uhamiaji.

Mahakama iliamuru Miguna arudishwe pasi masharti lakini alipokanyaga JKIA Jumatatu saa nane unusu alasiri, hakuruhusiwa kuondoka JKIA na sarakasi na kizaazaa kikaanza hadi sasa. Tamati ya kizugumkuti hiki ni Alhamisi.

You can share this post!

Diwani akanusha mashtaka 6 ya ulaghai Murang’a

Miguna apokea matibabu jijini Dubai baada ya maumivu kumzidi

adminleo