• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
KINAYA: Jenerali Miguna, japo mkali kama chui bado binadamu, baba ya mtu

KINAYA: Jenerali Miguna, japo mkali kama chui bado binadamu, baba ya mtu

Na DOUGLAS MUTUA

MOJAWAPO ya picha alizopigwa ‘Jenerali’ Miguna Miguna akiwa korokoroni juzi imenipa mtihani wa kutafakari.

‘Jenerali’ huyo wa vuguvugu la kufikirika liitwalo National Resistance Movement (NRM – of Kenya) alionekana amesimama karibu na ukuta, nyuma yake mkiwa na picha ya simba.

La ajabu ni kwamba – kutokana na ukubwa wa picha ya simba – ilionekana kana kwamba simba akimkodolea macho Miguna kwa mshangao.

Japo kibinadamu nilimwonea imani kidogo Miguna Miguna, sikujizuia kuangua kicheko nilipotafakari uwezekano wa simba kumshangaa.

Ikiwa kweli simba ndiye mfalme wa porini asiyetishiwa na yeyote, utakuwa mkali wa mambo ikiwa utamshangaza au kumshtua kwa chochote.

Nilijiuliza, iwapo hiyo ni ithibati kwamba ‘Jenerali’ Miguna Miguna ni mkali wa kuogopwa hata na mfalme wa porini.

Ina maana kwamba Miguna angeamua kuwa mnyama, basi angetwaa mamlaka ya ufalme wa porini kutoka kwa simba, au labda waunde serikali ya mseto! Usinidhani kichaa mwanangu, ningali timamu.

Ikiwa ‘Baba’ na Ouru walisalimiana na kuamua uadui wa tangu kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka jana uishe, mbona Miguna na Mfalme Simba wasifanye hivyo?

Ikiwa ‘Baba’ na Baba Jimmy waliunda serikali ya mseto baada ya kura za ‘Baba’ kuibwa peupe mnamo 2007, wakatuongoza mpaka 2013, Miguna na Mfalme Simba watakosaje?

Kumbuka Miguna hamjala swara wa Simba, naye Simba hamjala dagaa wa Miguna. Huo ungekuwa muungano mzuri sana wa wasiohasimiana kwa chochote.

Porini kungepatikana amani, angaa miongoni mwa wala-nyama na wala-nyasi kwa maana Miguna angewatetea wala-nyasi huku simba akiwatetea wala-nyama.

Kitega uchumi cha ulimwengu huo wa kusadikika kingekuwa mkorogo wa udongo na maji, kila mmoja ale kimyakimya bila kumsumbua mwenzake, mradi waishi kwa amani.

Binadamu pia wangefaidika pakubwa kwa maana swara wangeongezeka mno kwa kutoliwa na simba; tukitaka nyama tuwe tukimjulisha Miguna tu, naye akituma swara kuja kwetu kuliwa. Maisha ya raha hayo, au sio?

Kwa bahati mbaya, yote hayo ni ya kufikirika! ‘Jenerali Mwitu’ Miguna, japo mbishani na mkali kama chui aliyeliwa mwana, ni binadamu.

Na ana haki zote za binadamu. Hata ikiwa humpendi, ulizonazo anazo, huwi bora kumzidi, sote viumbe wa Mungu, hukumu yetu ni moja siku ya kiama.

Wajuaji watakwambia alikosea pakubwa kwa kutowapa paspoti yake maafisa wa uhamiaji kwenye uwanja wa ndege wa JKIA ili itiwe mhuri. Hiyo ndiyo sheria, sikatai.

Lakini naomba tu tuulizane hapa: nani aliyeiambia serikali kwamba ndiyo pekee iliyo na mamlaka ya kuvunja sheria na kudharau maagizo ya mahakama?

Singependa kuishi katika nchi isiyotawaliwa kwa sheria na singekuhimiza uvunje sheria yoyote. Lakini ningetaka kutawaliwa kwa kuonyeshwa kwa vitendo jinsi ya kutii sheria, yaani watawala wawe mifano bora kwangu.

Ni kwa mintaarafu hii ambapo nimemwandikia waraka Jaji Mkuu David Maraga – kabla ya kutimuliwa kwake maanake naamini kwaja – atushauri iwapo tutaanza kufungia nyama karatasi za maagizo ya mahakama.

Kisa na maana? Zimekuwa nyingi kama magazeti makuukuu na hazitumiki kwa vyovyote, mbona tusizitafutie matumizi mapya na bora?

[email protected]

You can share this post!

Wakenya wengine 20 watimuliwa Amerika

TAHARIRI: Ukatili wa polisi dhidi ya waandishi ulikiuka haki

adminleo