• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
JAMVI: Huenda ushirikiano mpya wa Raila na Uhuru ukamfaa pakubwa Moi

JAMVI: Huenda ushirikiano mpya wa Raila na Uhuru ukamfaa pakubwa Moi

Na WANDERI KAMAU

HUENDA muafaka wa kisiasa ulioafikiwa hivi majuzi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga ukageuka “baraka” kuu kwa Seneta Gideon Moi wa Baringo huku anapoweka mikakati ya kuwania urais 2022.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wasema huenda mpango wa huo ukawa ni njama kati ya familia za Kenyatta na Odinga kuendeleza “udhibiti wao wa kisiasa” nchini, kwa kumtumia Bw Moi, ikizingatiwa wawili hao wanajiandaa kung’atuka siasani.

Aidha, wanasema kuna uwezekano familia hizo mbili zinamchukulia Bw Moi kama anayeweza kulinda maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi, akilinganishwa na Naibu Rais William Ruto, ambaye pia anakamia urais kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).

“Kuna uwezekano muafaka huo unalenga kuunga mkono azma ya kisiasa ya Bw Moi kuwania urais, ikizingatiwa kwamba ni mmoja wao. Wanahitaji mmoja wao uongozini, ili kuwalinda, hasa dhidi ya kuhangaishwa kisiasa,” asema Bw Ndegwa Njiru, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Asema huenda hiyo ndiyo sababu kuu imechochea Uhuru na Raila kudumisha kimya kingi kuhusu muafaka huo, licha ya kushininikizwa na baadhi ya washirika wao wa karibu kuelezea waziwazi waliyoangazia katika mazungumzo hayo.

“Kilicho wazi hapa ni kwamba, huu ni muafaka unaoangazia maisha ya baadaye, viongozi hao watakapoondoka madarakani. Wanataka kumfadhili mgombeaji atakayewalinda wao binafsi, familia zao, biashara zao kati ya maslahi mengine muhimu,” asema Bw Njiru.

Wachanganuzi wasema kimantiki, hali hiyo ni sawa na ile iliyochochea Bw Kenyatta kujitosa siasani mnamo 1997, licha ya kutopenda kwake, huku msukumo ukiwa kulinda maslahi ya familia yake.

“Bw Kenyatta alishawishiwa kujitosa siasani 1997 na Rais Mstaafu Daniel Moi ili kuwa mlinzi wa kisiasa wa familia zao (Moi) na Kenyatta. Hii ni licha ya Bw Kenyatta kutopendelea siasa,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU.

Wanasema kung’aa kwa nyota ya kisiasa ya Bw Kenyatta hadi kuwa rais kunatokana na juhudi za pamoja za Mzee Moi na Mama Ngina Kenyatta, kuhakikisha “Bw Kenyatta angekuwa  katika nafasi ambapo angeweza kulinda maslahi yao.”

 

Kufuata Mzee Moi

Asema: “Katika kipindi ambacho Bw Kenyatta amekuwa uongozini, ameonekana kama kivuli cha mamake (Mama Ngina). Hii ni sawa  na Gideon (Moi) ambaye amekuwa akifuata kwa umakinifu mkubwa misimamo anayotaka babake (Mzee Moi).”

Wanaeleza kwamba, kama Bw Kenyatta, Bw Moi atakuwa “kivuli” cha familia hizo, ikiwa ataibuka kuwa rais.

Madai hayo pia yalitolewa na baadhi ya viongozi wa ukanda wa Magharibi, ambao wamemlaumu Bw Odinga kwa “kuwasaliti” kwa kubuni muafaka huo.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Bonny Khalwale, alisema muafaka huo ni “zaidi ya viongozi wa NASA” kutohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Bw Odinga mnamo Januari 30 kama “Rais wa Wananchi.”

“Muafaka huo hauhusiani kamwe na kutojitokeza kwa Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Kalonzo Musyoka (Wiper)  katika hafla ya Bw Odinga. Unaangazia uendelezaji wa ukiritimba wa kisiasa wa familia za Odinga, Kenyatta na Moi, ambazo zimekuwa uongozini tangu 1963,” akasema Dkt Khalwale.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wameonya kuhusu hatua hiyo, wakishikilia kwamba utakuwa usaliti mkubwa wa Bw Kenyatta dhidi ya Bw Ruto, ikizingatiwa ameonyesha uzalendo mkubwa kwake kuanzia 2013, alipoanza kuhudumu kama Naibu Rais.

Wanaeleza kwamba, ingawa mkataba uliopo ni wa hao wawili, ufasiri wake ni kwamba Bw Kenyatta, na jamii za GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru) kwa jumla, zina “deni” la kisiasa ambalo lazima zilipe kwa Bw Ruto.

 

Uasi

“Ikiwa hiyo ndiyo siri iliyofichika kwenye muafaka huo, basi Rais Kenyatta atakuwa analifarakanisha eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa, hali ambayo itazua uasi mkubwa wa kisiasa,” aonya wakili Wahome Kiruma.

Tayari, kumeibuka ripoti kwamba kuna mazungumzo ya kichinichini yanayoendelea kati ya viongozi wa Magharibi na Bonde la Ufa, kumrai Bw Ruto kubuni ushirikiano mpya wa kisiasa na Bw Mudavadi kama njia moja ya “kukabili usaliti” wa Bw Odinga.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wamejitokeza wazi kutetea muungano wa Rais Kenyatta na Bw Ruto, wakiutaja kama ndoa ambayo haiwezi “kusambaratishwa na yeyote.”

Miongoni mwao ni mbunge wa Gatundu Moses Kuria, Gavana Ferdinard Waititu na Mbunge, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege, ambao wametaja dhana hizo kama “uvumi usio na msingi wowote.”

“Kilicho wazi hapa ni kwamba, kuna jaribio na kila njia ya kuwakosanisha Rais Kenyatta na Bw Ruto kabla ya 2022. Haya ni mambo tunayoyatarajia. Hata hivyo, tunawahakikishia washindani wetu kwamba, mpango ni ule ule, kwamba mgombea mkuu wa JP ni Bw Ruto,” akasema Bi Chege.

You can share this post!

JAMVI: Muafaka ulivyoyeyusha siasa kali za Raila na NASA

JAMVI: Raila njiapanda huku wandani na wafuasi wakitilia...

adminleo