• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Walimu waliotumwa kufundisha maeneo hatari walia kukosa mshahara

Walimu waliotumwa kufundisha maeneo hatari walia kukosa mshahara

Bw Kedi Abdulrahman Guyo, mmoja wa walimu wanaofundisha kwenye Wadi ya Basuba, katika shule ya Kiangwe. Aanasema tangu serikali iwapeleke kuhudumu kwenye shule hizo, hakuna malipo yoyote wamepewa kwa miezi minne sasa. Picha/Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kitaifa imeelekezewa kidole cha lawama kwa kuwatelekeza walimu wanane iliyotangaza kuwaajiri mapema mwaka huu ili kuhudumia shule tano za wadi ya Basuba, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Shule hizo za msingi ambazo ni Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe, zilikuwa zimefungwa tangu mwaka 2015 kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Aidha Januari 2018, serikali iliagiza shule hizo kufunguliwa upya baada ya kutoa nafasi nane za ajira kwa vijana wa jamii ya Waboni waliohitimu masomo ya kidato cha nne ili kusomesha kwenye shule hizo.

Katika kikao na wanahabari Jumanne, walimu hao walifichua kuwa tangu serikali ilipowatuma kufundisha kwenye shule husika, hakuna mshahara wowote ambao wamepokea kama ilivyokuwa imeahidiwa.

Msemaji wa walimu hao, Bw Kedi Abdulrahman Guyo, alisema serikali haijatoa mwelekeo wowote kuhusiana na ajira yao.

Bw Guyo pia aliikashifu serikali kwa kukosa kushughulikia miundomsingi ya elimu kwenye shule hizo hasa tangu ilipowaajiri walimu hao.

“Sisi tunateseka. Tangu tulipopelekwa Basuba, hakuna mtu ambaye amekuja kutuangalia. Shule pia zimetelekezwa. Hakuna chaki wala vitabu vya kufundishia. Tangu Januari hadi sasa ni Aprili, mshahara hatujapewa wala hakuna mtu aliyetuongelesha juu ya mwelekeo wa mambo. Tungeomba serikali itueleze ni nini hasa imetupangia,” akasema Bw Guyo.

Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, Deko Barissa wakati wa mahojiano na Taifa Leo mjini Lamu. Anaitaka serikali kusuluhisha mgogoro uliopo wa kukosa kuwalipa walimu wanaohudumia shule za wadi ya Basuba, Lamu Mashariki. Picha/Kalume Kazungu

Baadhi ya walimu pia walilalamika kuwa wanalazimika kuishi maisha magumu ilhali wengine wakilazimika kulala njaa kwa zaidi ya siku mbili mfululizo.

“Mara nyingi tunalazimika kula chakula kwenye kambi za jeshi na polisi ambao wanaendeleza operesheni ya Linda Boni.

Familia zetu zinahangaika. Tumekuwa tukiulizwa fedha tunazofanyia kazi ziko wapi ili kukimu mahitaji kwa familia zetu. Wengi wetu tuko na wake na watoto wanaohitaji kutunzwa,” akasema mmoja wa walimu hao ambaye alidinda kutajwa jina.

Naye Mwakilishi wa Wadi ya Basuba, Bw Deko Barissa, aliitaka serikali kutimiza ahadi ya awali ya kuwapa mishahara walimu hao ili kujikimu maishani.

Alisema vijana hao wamekuwa wakihatarisha maisha kwa kujitolea kuhudumu kwenye eneo ambako usalama umekuwa ukitiliwa shaka.

 

Kuchezewa shere

“Tunahisi serikali inatuchezea shere sisi Waboni. Wanaagiza vijana wetu kuhudumia shule zetu na kisha hawawalipi. Shule zenyewe zimetelekezwa. Hakuna vitabu. Chaki pia ni shida.

Wanafunzi hata hawasomi ilhali serikali inaendelea kujipiga kifua kwamba shule za Basuba zimefunguliwa.Serikali iwalipe hawa vijana. Basuba ni eneo linalojulikana kwa mahangaiko na utovu wa usalama unaochangiwa na Al-Shabaab. Tumechoka kuchezewa,” akasema Bw Barissa.

Kamishna wa kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri aidha hakupokea simu wala kujibu ujumbe uliotumwa kuhusiana na suala hilo.

Aidha Naibu Kamishna wa Lamu, Bw Louis Rono, alisema suala kuhusiana na walimu wa Basuba lilistahili kujibiwa vyema zaidi na idara ya elimu ya kaunti ya Lamu.

“Itakuwa bora ukiwapigia wakurugenzi wa elimu wa kaunti ya Lamu. Ninaamini wao wako na jawabu mwafaka kuhusiana na suala hilo,” akasema Bw Rono.

Kwa upande wake aidha, Afisa Mwelekezi wa Idara ya Elimu wa Kaunti ya Lamu, Bw William Micheni, alisema katu hahusiki na matatizo ya walimu wa Basuba.

“Mimi sijafahamu ni nani hasa aliyewaajiri walimu hao na pia mimi si afisi ya kamishna wa Kaunti,” akasema Bw Micheni.

You can share this post!

Yaya mlishwa makombo atafuna mayai ya mdosi

Korti za Kenya ni nzuri ajabu, raia wa Burundi asema baada...

adminleo