• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
MAKALA MAALUM: Wanawake wanavyooana kuepuka utasa

MAKALA MAALUM: Wanawake wanavyooana kuepuka utasa

NA PETER MBURU

UTASA na ugumba ni hali inayosababisha uchungu kwenye nyoyo za wanandoa, mbali na kushusha hadhi na heshima na tamaduni za kiafrika hazijakuwa zikichukulia suala hili kwa wepesi.

Japo si mapenzi ya mtu kukosa watoto, mawili haya yanapobisha hodi maishani, huwa ndio mwanzo wa giza na mara nyingi huzaa utengano.

Kwa wanawake wa Emurua Dikirr, Kaunti ya Narok haswa, hali hiyo au ile ya kukosa watoto wa kiume ni suala linalochukuliwa kwa uzito sana kwa muda mrefu na limezaa ndoa za aina yake kama njia ya kutibu upweke unaombatana na hali hizo.

Wakaazi hao,  ambao wengi wao ni wa kutoka jamii ya Kalenjin kwa miaka mingi wamekuwa wakiendesha ndoa baina ya kina mama, kwa wanawake wasio na uwezo wa kuzaa au wanaokosa kufanikiwa na watoto wa kiume.

Tulipowatembelea kina mama hao tulibaini kuwa ndoa hizo ambazo zimeruhusiwa na itikadi za jamii ya Kalenjin zimekuwa zikiendeshwa tangu jadi na kuwa huongozwa na wazee wakamilifu walioteuliwa na jamii.

Aidha ili kudhihirisha mapenzi kwa anayetaka kumwoa (mke), mwanamke anayeoa (mume) hulipia mahari kabla ya kuruhusiwa kwenda kuishi naye.

Kutana na Bi Esther Simatei, 86, kutoka kijiji cha Tagitech, eneobunge la Emurua Dikirr na ambaye amekuwa kwenye ndoa na Mzee William Tuwei, 98, kwa zaidi ya miaka 60 sasa.

Bi Esther Simatei, 86 akiwa na mkewe Bi Nancy Chepkorir, 47. Picha/ Peter Mburu

Hata hivyo, kwa muda huo wote wanandoa hao hawajawahi kubarikiwa na mtoto kutokana na hali ya ugumba iliyowakumba.

Ni pengo hilo lililompelekea Bi Simatei kuchukua hatua ya kipekee mnamo 1984 ili kukidhi kiu cha kuitwa mzazi alipoamua kumuoa mwanamke mwenzake awazalie watoto.

“Ni mila na itikadi zetu kuwa ikiwa mama hana uwezo wa kuzaa ama ameshindwa kupata mtoto wa kiume baada ya majaribio mengi anaweza kuoa mama mwenzake kwa ajili ya kutatua hali hiyo,” Bi Simatei akasema.

Ni itikadi hii iliyompelekea Bi Simatei kuiamsha sheria hiyo ya kitamaduni kufanya kazi kwa msaada wake na hapo akafunga pingu za maisha na Nancy Chepkorir, wakati huo akiwa na miaka 14 pekee.

 

Harusi

Sherehe za harusi ya kitamaduni ziliandaliwa baada ya Bi Simatei kumlipia ‘mkewe’ mpya mahari na kuanzia hapo, mustakabali wa ndoa wa Bi Chepkorir, 47, ukafungwa mara moja.

Aliingia kwenye ndoa hiyo akiwa bikira, lakini sasa Bi Chepkorir ana watoto wanane, baada ya mmoja kuaga dunia.

“Sikuwa na mtoto hata mmoja, hata sikuwa na uzoefu wowote wa mapenzi lakini sasa nimezeeka nikiwa mke wa mwanamke mwenzangu,” Bi Chepkorir akasema.

Kwenye kisa kingine Bi Rael Too, 86, anayetoka kwenye kabila dogo ya Kipsigis alifunga ndoa sawia na wanawake wawili, baada ya mumewe kufariki mnamo 1991.

Bi Too aliishi eneo la Tororet, Narok mbeleni lakini akahamia Emurua Dikirr baada ya mumewe kufa. Japo walibarikiwa na wasichana watano, ajuza huyu hakuridhika kwa kukosa watoto wa kiume na hivyo akaamua kuoa ili kukidhi matakwa yake.

Elizabeth Arap Boiyon,72 (kushoto) akiwa na ‘mkewe’ Helen Chebet ambaye pia ni bintiye walipohojiwa na Taifa Leo. Picha/ Peter Mburu

Kuziba pengo

“Nilikuwa na watoto watano wasichana lakini bado kulikuwa na pengo moyoni mwangu kutokana na kukosa wavulana, nilijua ningebaki na upweke baada ya mabinti zangu kuolewa,” Bi Too akasema.

Kutatua upweke wa nafsi, aliendelea kuoa wanawake wawili mnamo 1996 na 2003 ili kuzaliwa watoto wengi wa kiume, ambao kulingana naye wangekuwa ulinzi wake uzeeni.

“Nilianza kufanya uchunguzi wa mwanamke mwenye tabia nzuri na sifa za mkema mwema kijijini, baada ya muda mfupi nilipata na nikamwomba mkono kwenye ndoa. Vivyo hivyo niliweza kuoa Lilian mnamo 1996 na Valentine-2003,” Bi Too akasema.

Bi Too alieleza kuwa kabla ya taratibu za ndoa kuanzishwa, aliwatuma marafiki zake kumwitia wake hao kisha akaelezea mapenzi yake kwao nao wakakubali na kudhihirisha kumpenda pia.

Akishajiishwa na hamu ya kupata watoto wavulana ili kuwa kwenye nafasi ya juu katika jamii, Bi Too aliendelea kushuhudia wake zake wakipata zaidi ya watoto 12, wanane kati yao wavulana.

Hii ni kando na kuwa ni majirani wa karibu sana na mbunge wa eneo hilo, Bw Johanna Ng’eno ambaye pia amekuwa akisukumwa na familia na wanajamii kuoa, baada ya kusalia kapera akiwa na miaka 45.

Rael Too, 86 (kushoto) akiwa na ‘mkewe’ Valentine Too, 39 wakati Taifa Leo iliwatembelea kwa nyumbani. Picha/ Peter Mburu

Kuokoa jahazi 

Kulingana na Mzee wa jamii ya Kalenjin, Bw Kibet Arap Tanui tamaduni za ndoa baina ya wanawake zimekuwa zikiendeshwa tangu uzawa na zimewasaidia wanawake wengi tasa na waliokosa wavulana kuokoa majahazi ya ndoa zao yasizame.

“Huu ni utamaduni ulioingizwa ili kuwasaidia wanawake wa aina hiyo kujihisi kama wenzao wenye uwezo wa kuzaa. Anachohitaji mwanamke ni kutafuta mwanamume wa kumzalia watoto na mke anayeoa tu,” akasema mzee Tanui.

Alisema kuwa mwanamume anayehusika kwenye tendo la kuzaa watoto hana haki kudai watoto hao kwani analipwa kufanya hivyo kwa misingi ya mifugo.

Ndoa hizi hata hivyo hazijagusiwa vyema na sheria ya ndoa ya 2014 ambayo ndiyo huelekeza aina za ndoa zinazoruhusiwa kisheria.

Wakili wa masuala ya familia Bw Steve Biko asema kuwa ndoa hizo zinazoitwa ‘ndoa za Toloita’ zinatambuliwa na sheria, japo akihoji kuwa zinakumbwa na hatari ya kupotea kutokana na ustaarabu wa siku hizi ulioletwa na tabia ya watu kumiliki watoto wasio na familia (adoption).

“Ni ndoa zilizosaidia sana lakini sasa kimekuwa kitendawili cha ng’ombe na maziwa, kina mama wa aina hiyo sasa wanajiuliza mbona waoe kupata watoto wakati wanaweza kupata watoto bila kuoa,” wakili huyo akahoji.

You can share this post!

SHANGAZI: Iweje wananishuku ilhali ‘mali’ nimetia...

TAHARIRI: Maagizo ya korti hayafai kupuuzwa

adminleo