• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
WATOTO: Bingwa wa uogeleaji

WATOTO: Bingwa wa uogeleaji

Na PATRICK KILAVUKLA

SIRI ya kufualu kuwa muogeleaji mahiri ni kufuata maagizo ya mkufunzi wa taaluma ya kuogelea kwani, si fani hatari sana ukiyazingatia.

Pamoja na hayo, yakupasa uwe mjasiri na kufanya mazoezi ya kila Mara kujifahamisha na hali ya angaa na mbinu kabambe za uogeleaji. Isitoshe, ni mchezo humweka muogeleaji kimwili na kisaikolojia fiti.

Ushauri huu ni wa muogeleaji chipukizi hodari Sharon Ngami,10, darasa  la nne shule ya msingi ya Visa Oshwal,Westlands.

Ngami anasema ilimchukua wiki tatu hivi kuanza kujua kuogelea na hata sasa anashiriki mashindano kujipa upevu zaidi na hata amewahi kushinda na kutuzwa.

Muogeleaji chipukizi Sharon Ngami,10, wa darasa la nne Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Nairobi baada ya kutuzwa. Picha/Patrick Kilavuka

“Baada ya mwalimu wangu wa uogeleaji George Juma kuona ari ambayo nilikuwa nayo wakati tulikuwa tunajinoa, aliamua kuniweka kwenye mizani ya mashindano ambayo yalifanyika shuleni mwetu na nilifanya kweli kwa kuwa mshindi wa mtindo wa Free Sytle na Backstroke,” anasema muogeleaji huyo ambaye ana medali ya dhahabu na shaba kwenye kabati lake.

Baada ya mwalimu wake kumwaminia zaidi alimpa nafasi nyingine ya kushiriki Swimming Gala ambayo ilifanyika shule ya Makini na kuibuka wa nne bora. Hata hivyo, anasema mashindano hayo yalimpa changamoto zaidi ya kujibidisha zaidi kujinoa ili aendelea kutesa.

Muogeleaji chipukizi Sharon Ngami,10, wa darasa la nne Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Nairobi akiogelea. Picha/Patrick Kilavuka

Ngami hufanya mazoezi yake wakati wa mapaumziko shuleni na wakati wa somo la fani hiyo shuleni.

“Ninapenda kuwa makini wakati tunapata mafunzo kuhusu mchezo huu na yamenisaidia kufanya vyema wakati tunaposhiriki mashindano,” anakiri muogeleaji chipukizi Ngami ambaye ana kiu ya kufanya vyema siku za usoni katika fani hii ambayo anaihusudu.

Uraibu wake ni kuchora na kuimba na angependa kuwa dakari siku zijazo kwani, mtima wake hupenda kuona afya ya watu ikiwa shwari ili waafikie malengo yao maishani.

Muogeleaji chipukizi Sharon Ngami,10, wa darasa la nne Shule ya Msingi ya Visa Oshwal, Nairobi akifanya mazoezi ya kuogelea. Picha/Patrick Kilavuka

Kwa vile hamna barabara ndefu ambayo haikosi kona, chipukizi huyo anasema tatizo lake huwa kutetema wakati maji yanakuwa baridi sana au msimu wa baridi.

Ujumbe kwa waogeleaji chipukizi ni kwamba, wasiogope na wawasikize walimu wao na wajifunze kutoka kwa waogeleaji mahiri watangulizi.

You can share this post!

Buffon: Michael Oliver ana jaa la taka rohoni, alifaa kula...

‘Baba’ akutana na Mzee Moi

adminleo