• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Afueni kwa vijana bunge kuwaondolea visiki vya kupata ajira

Afueni kwa vijana bunge kuwaondolea visiki vya kupata ajira

Na CHARLES WASONGA

BUNGE Jumatano lilipitisha hoja inayopendekeza kupiga marufuku vijana kutozwa ada ya kulipia vyeti vinavyohitajika wanapotafuta kazi.

Vyeti hivyo ni pamoja na kile cha kuonyesha mtu ana nidhamu na hana rekodi ya uhalifu, cheti cha kuonyesha hadaiwi na Bodi ya Elimu ya Juu (HELB), kwamba ana maadili, cheti cha kuonyesha kwamba analipa madeni yake na kwamba hulipa ushuru.

Cheti cha kwanza hulipiwa katika makao makuu ya CID na hujulikana kama “Certificate of Good Conduct”.

Wabunge walikubliana na Mbunge Mwakilishi wa Nyandarua, Bi Faith Gitau, kwamba, kijana wa umri wa kati ya miaka 18 na 35 asiye na kazi hawezi kupata pesa za kulipia vyeti hivyo ambavyo gharama yake ni Sh4,500.

“Vijana waliomaliza masomo, wengi wao kutoka familia maskini hawawezi kupata kiwango hicho cha fedha ili waweze kugharamia vyeti hivyo. Hitaji hili ni kama kuwaadhibu vijana ambao huhangaika kila mara wakisaka ajira. Serikali iondoe ada hizi ili vijana waweze kupata stakabadhi hizo bila gharama yoyote,” akasema.

Kupitia hoja hiyo, Bi Gitau anaitaka serikali iwape vijana vyeti hivyo bila malipo.

Pia, anaitaka Serikali iharakishe mpango wa kuanzisha Halmashauri ya Kitaifa ya Ajira (NEA).

Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu, alisema kwa kuwa ni wajibu wa serikali kuwasaidia vijana kusaka ajira, taasisi za serikali hazipaswi kuwatoza ada zozote wanazohitaji kufanikisha shughuli hiyo.

“Iweje ajenda kuu ya serikali ni kuhakikisha kuwa vijana wanapata ajira, lakini kwa upande mwingine taasisi zake zinaweka vizingiti kwa kuwatoza ada ili kupata stakabadhi hizi za kimsingi? “akauliza mbunge huyo wa chama cha Jubilee.

 

Ajira ng’ambo

Nao Wabunge Cecily Mbarire (Maalum) na David Gikaria (Nakuru Mashariki) waliitaka serikali kukusanya maelezo ya vijana wote waliomaliza masomo, ili iweze kutekeleza mpango wa kuwatafutia ajira humu nchini na hata ng’ambo.

“Baada ya kuwatoza vijana ada kama hizi, serikali ianzishe halmashauri ambayo itakusanya data kuhusu vijana wote wanaokamilisha masomo kila mwaka ili wizara husika iweze kuwasaidia” akasema Bw Gikaria.

Kutokana na kupitishwa kwa hoja hiyo bungeni, sasa ni wajibu wa kamati ya Bunge inayohusika na utekelezaji wa sheria kufuatilia na kuhakikisha kuwa jambo hilo linatekelezwa.

Kinyume na mswada ambao unapopitishwa na Bunge hupelekewa rais kutia saini, hoja ikipitishwa huwa tayari ni sheria, lakini yafaa kufuatiliwa kwa utekelezaji wake.

Na punde baada ya wenzake kupitisha hoja yake, Bi Gitau alisema atahakikisha kuwa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia inaitekeleza kikamilifu.

You can share this post!

Hakimu aachilia washukiwa akisema ‘Nimewaachia...

Wamiliki wa shule za kibinafsi waionya Serikali

adminleo