• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 12:50 PM
Malori yenye magunia 330 ya makaa yanaswa

Malori yenye magunia 330 ya makaa yanaswa

Na OSCAR KAKAI

MAAFISA wa misitu na wa serikali ya kaunti wamenasa malori matatu yakisafirisha magunia 330 ya makaa mjini Kacheliba, kaunti ya Pokot Magharibi.

Malori mawili ambayo yalikuwa yakihusika na biashara hiyo kinyume na sheria yenye nambari za usajili KXF 25 L, KBJ 608 Q, kwa sasa yako katika ofisi za huduma ya misitu mjini Kapenguria huku moja limekwama barabarani eneo la Kacheliba baada ya kuharibika likiwa njiani kutokana na mvua kubwa inayonyesha katika eneo hilo.

Afisa anayesimamia misitu katika kaunti, Bw Allan Ongere, alisema maafisa waliokuwa wakishika doria walinasa malori hayo kufuatia agizo la siku tisini la serikali kusimamisha ukataji miti ili kuokoa misitu nchini.

Bw Ongere alisema kuwa watu sita ambao wanahusika na biashara hizo za makaa wamejisalimisha na watapelekwa mahakamani leo Jumatatu.

“Madereva wa malori hayo walihepa baada ya kuvamiwa na maafisa lakini wenye malori hayo wamejisalimisha kwetu. Maafisa wa misitu wanalinda lori moja ambalo limekwama,” alisema.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia simu, afisa wa Mazingira na Maliasili katika kaunti hiyo, Bw Peter Adoki, alisema kuwa walisimamisha malori hayo ambayo yalikuwa yakibeba makaa kutoka eneo la Kanyerus kuelekea mjini Kisumu wakiwa kwenye msako kisha wakayashika.

“Tuliwavamia baada ya kuona malori hayo yakiwa yamebeba makaa. Askari wa akiba na machifu walitusaidia kushika malori hayo,” alisema.

Bw Adoki alisema kuwa watu wengine kumi wamenaswa eneo la Kanyarkwat na askari wa akiba wakisafirisha magunia 34 ya makaa baada ya kupashwa habari na wakazi.

Afisa huyo aliwaonya wakazi kuhusu ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa kwenye misitu ya serikali kwenye kaunti hiyo akisema kuwa wale watapatikana watakabiliwa na mkono wa sheria.

“Serikali imesimamisha uchomaji wa makaa na hatutaruhusu mtu yeyote kukata miti kiholela sababu tutanatekeleza agizo hilo. Wiki mbili ambazo zimepita tumeshika lori tatu zikisafirisha mbao na hatutacheka na wale ambao wanaharibu miti.

Alisema kuwa biashara za makaa zinafaa kusimama kwa wakati huu hadi muda wa agizo kuisha Mei 2.

“Kama serikali ya kaunti tutatoa mwelekeo baada ya tarehe hiyo lakini hatutaruhusu biashara ya makaa isipokuwa ya kutumika nyumbani. Kwa sasa tunakuwa wakali kwa wale wanaenda kinyume na agizo la siku tisini kuhusu ukataji miti,” alisema Bw Adoki.

 

You can share this post!

Onyo kwa wanaouza dawa za hospitali za umma

Raila akamilisha ziara ya kumwakilisha Uhuru Afrika Kusini

adminleo