• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
Kituo maalum cha watalii chazinduliwa Lamu

Kituo maalum cha watalii chazinduliwa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kaunti ya Lamu imezindua ujenzi wa kituo maalum cha mawasiliano  kwa watalii wote wanaozuru eneo hilo.

Waziri wa Utalii, Biashara na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu, anasema kituo hicho kinachobuniwa eneo la Manda kitatumiwa kukusanya taarifa kuhusu watalii na wageni wote wanozuru Lamu.

Bw Mwasambu alisema kituo hicho pia kitasaidia kutoa maelezo na maelekezo kuhusu sehemu mbalimbali ambazo watalii hao wangependa kutembelea wanapokuwa ziarani Lamu.

Akizungumza na Taifa Leo ofisini mwake Jumatatu, Bw Mwasambu alisema kumekuwa na tatizo la tangu jadi kuhusiana na miundomisngi duni ya kuutangaza utalii wa Lamu.

Alisema anaamini kuanzishwa kwa kitu hicho kutasaidia pakubwa kuutangaza utalii wa Lamu hata katika mataifa ya nje.

Waziri huyo alisema mara nyingi watalii wamekuwa wakikosa kufahamu sehemu za vivutio kwani hazijakuwa zikitangazwa.

Alisema kituo kitakachobuniwa kitawezesha watalii wenyewe kuchagua sehemu watakazotembelea kujifyurahisha kila mara wanapofika Lamu.

Kituo hicho pia kitatoa nafasi kwa watalii kutoa mapendekezo kuhusiana na jinsi wanavyofaa kuhudumiwa.

“Tumeamua kuanzisha kituo hicho maalum kama kaunti ili watalii wanaozuru eneo letu waweze kutoa ripoti zao kila mara wanapozuru eneo letu. Pia wataweza kupata matangazo kuhusu sehemu za vivutio ambazo zafaa kwa matembezi yao hapa Lamu.

Pia tunatarajia watalii wenyewe hasa kutoa mapendekezo ya jinsi wanavyofaa kuhudumiwa. Lengo letu hasa kama idara ya utalii ni kuboresha zaidi huduma zinazotolewa kwa watalii wetu na pia kuutangaza utalii wa Lamu kwenye mataifa ya nje,” akasema Bw Mwasambu.

Kituo hicho pia kitapunguza visa vya watalii wanaozuru Lamu kuibiwa na wahuni kwani ni katika kituo hicho ambapo maelezo na taarifa zote kuhusu vijana wanaotoa huduma za matembezi kwa watalii ufuoni vitapatikana.

“Tutahakikisha vijana wote wanaotoa huduma za ufuoni kwa watalii wetu hapa Lamu wako na leseni na ripoti kuwahusu tunazihifadhi kwenye kituo hicho.

Watalii wanaozuru Lamu watapata fursa ya kuchagua ni kijana yupi hasa atakayemchukua kusaidia katika matembezi yake. Hilo litasaidia visa vya watalii kuporya au kupotezwa,” akasema Bw Mwasambu.

You can share this post!

Uber kuwatuza madereva wake

Red Cross yawafadhili Waboni kwa biashara na kilimo

adminleo