• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wenye ardhi wataka wafidiwe

Wenye ardhi wataka wafidiwe

NA KALUME KAZUNGU

WAMILIKI wa ardhi zilizotengewa ujenzi wa kiwanda cha nishati ya upepo katika eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu wanamlalamikia mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuchelewesha fidia zao.

Wamiliki hao zaidi ya 600 ambao wengi wao ni wakulima, wameeleza kufadhaishwa kwao na kimya kinachoendelea licha ya ardhi zao kutwaliwa na miaka mitatu iliyopita kwa ahadi kwamba wangefidiwa ardhi hizo.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu kima cha Sh21 bilioni uko chini ya ufadhili wa kampuni ya kibinafsi ya Elicio kutoka Ubelgiji kwa ushirikiano na kampuni ya Kenwind Holdings ya hapa nchini.

Jumla ya keari 3,206 za ardhi tayari zimetengwa katika eneo la Baharini ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.

Wakizungumza na Taifa Leo kijijini Baharini jana, wakulima hao walisema wamekuwa wakinyimwa fursa ya kuchukua mikopo katika benki mbalimbali kwa kutumia hatimiliki za ardhi zao kwa madai kwamba ardhi hizo tayari zimefungishwa na mwekezaji wa mradi huo wa kawi ya upepo.

Wakulima hao waliwataka wahusika wa mradi huo kuwaeleza sababu inayopelekea kucheleweshwa kwa fidia zao.

“Tangu ardhi zetu kutwaliwa na mwekezaji wa mradi wa upepo, hatimiliki za ardhi zetu hazitufai. Kila benki imedinda kutuamini na kutupa mikopo. Wanasema ardhi yetu tayari iko mikononi mwa mwekezaji wa kiwanda cha upepo. Ombi letu ni mwekezaji kuharakisha fidia ili nasi tujiendeleze,” akasema Bw Zachariah Ng’ang’a.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Baharini, Bw Linus Gachoki, alishikilia kuwa wakulima wanaunga mkono kuanzishwa kwa mradi huo wa upepo eneo lao.

Alisema haelewi ni kwa nini kumekuwa na kucheleweshwa kwa fidia ya ardhi ambazo tayari zimekabiliwa mwekezaji wa kiwanda hicho.

“Wakulima wote hapa Baharini wanaunga mkono kuekezwa kwa kiwanda cha nishati ya upepo eneo letu. Hii ndiyo sababu tukaamua kukabidhi ardhi zetu kwa mwekezaji hasa baada ya kuahidiwa kwamba tungefidiwa. Tuelezwe kwa nini fidia hiyo imechelewa kutolewa,” akasema Bw Gachoki.

Kwa upande wake aidha, Afisa Msimamizi wa mradi huo, Bi Susan Nandwa, alisema mazungumzo yanaendelea kati ya mwekezaji na Tume ya Kawi nchini (ERC) kuhusiana na jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.

Aliwataka wamiliki wa ardhi za eneo la mradi kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa watalipwa fidia zao.

“Majadiliano bado yanaendekea kati yetu na ERC. Punde mradi utakapopasishwa katika awamu hiyo tutaanza mara moja shughuli ya kuwafidia wakulima. Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) tayari imepasisha mradi.

Wamiliki halisi wa ardhi pia wametambuliwa. Wakulima wasiwe na shaka. Tunawashughulikia,”akasema Bi Nandwa.

You can share this post!

Red Cross yawafadhili Waboni kwa biashara na kilimo

WATOTO: Japo walemavu, wamedhihirisha umahiri wao katika...

adminleo