• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 9:55 AM
Familia ya Moi iheshimiwe, viongozi waionya Jubilee

Familia ya Moi iheshimiwe, viongozi waionya Jubilee

Na WYCLIFFE KIPSANG

VIONGOZI wa chama cha Kanu katika eneo la Bonde la Ufa wamewataka wenzao wa Jubilee kuheshimu familia ya Rais Mstaafu Daniel Moi.

Viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat walikosoa wanasiasa wa Jubilee kwa kuingiza siasa katika ziara ya kinara wa NASA Raila Odinga nyumbani kwa Mzee Moi katika eneo la Kabarak wiki iliyopita.

Walishutumu madai yaliyotolewa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen kuwa juhudi za wendani wa Naibu wa Rais William Ruto za kutaka kukutana na Mzee Moi zimegonga mwamba.

“RaisMstaafu anahitaji heshima. Bw Murkomen anastahili kujua kuwa Mzee Moi ni sawa na taasisi na kuna hatua zinazofaa kufuatwa ili kukutana naye,” akasema Bw Salat.

“Seneta Murkomen ndiye alifaa kuwa wa kwanza kumtembelea Mzee Moi zamani kwa sababu yeye ndiye alimlea kisiasa, lakini hakufanya hivyo. Wasiwasi wetu ni kuwa anatafuta nini kwa Mzee Moi wakati huu,” akaongezea.

Seneta Murkomen wikendi iliyopita alisema juhudi zao za kutaka kukutana na Rais Mstaafu Moi zimegonga mwamba kwa sababu mwanawe Seneta wa Baringo Gideon Moi hataki.

Mwenyekiti wa chama cha Kanu Kaunti ya Kericho Joseph Soi alidai kuwa viongozi wa Jubilee wanapanga kumzuia Bw Gideon Moi kutowania urais 2022.

“Hakuna makosa kuwa na viongozi wawili kutoka jamii ya Wakalenjin wakiwania urais,” akasema Bw Soi.

Bw Odinga, wiki iliyopita, alimtembelea Mzee Moi na akapokelewa na Bw Gideon Moi, wabunge William Kamket (Tiaty) na Silas Tiren (Moiben) na Bw Salat.

You can share this post!

WATOTO: Japo walemavu, wamedhihirisha umahiri wao katika...

COTU na FKE zatisha kujiondoa NSSF

adminleo