• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
SHAIRI: Buriani Matiba, ulazwe pema peponi

SHAIRI: Buriani Matiba, ulazwe pema peponi

Na KULEI SEREM

Nimetingwa na huzuni, nimepokea habari,
Inanichoma moyoni, kama moto msumari,
Shujaa wetu jamani, ametuaga kwaheri,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Wakenya twaomboleza, kwa hakika tunalia,
Nimekuwa nikiwaza, ukweli taka kujua,
Habari zikaeleza, ya kwamba aliugua,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Ni wa vyama vingi baba, alitengeneza njia,
Kaumia awe tiba, kuleta demokrasia,
Jasiri yule Matiba, sasa ametangulia,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Kama cha puani chuma, alikuwa ni imara,
Kidete alisimama, akatuonyesha dira,
Aliziongoza vyema, alizoshika wizara,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Wakati wa uwaziri, kaleta mabadiliko,
Alikuwa ni jasiri, tena mwenye ongezeko,
Licha kuwa mashuhuri, kapata masikitiko,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Mateso ya gerezani, na wale watu watesi,
Alitiwa mikononi, bila kustahili kesi,
Aliumia kichwani, kapatwa na kiharusi,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

Kwaheri wetu jagina, makiwa! Kwa familia,
Sijui ila Rabana, yeye mwenyewe ajua,
Mioyoni lako jina, daima litabakia,
Ni buriani Matiba, ulazwe pema peponi.

You can share this post!

Shirika lasaka wanaume 100 kushiriki mpango wa kupanga uzazi

Waililia serikali kuwanasua kutokana na minyororo ya pombe...

adminleo