• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
Wakazi wakwama juu ya miti kufuatia mafuriko

Wakazi wakwama juu ya miti kufuatia mafuriko

STEPHEN ODUOR na JADSON GICHANA

WAKAZI wa eneo la Nanigi, Kaunti ya Tana River, wamekuwa wakiishi mitini na kwa paa za nyumba zao kwa siku tatu zilizopita baada ya nyumba hizo kujaa maji ya mafuriko. Wakazi hao ambao waliamshwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha usiku, walilazimika tena kukesha bila chakula kabla serikali ya kaunti kutuma boti la kasi kuwaokoa.

“Hatukuchoka kupiga simu ili watu waje kutusaidia. Waliokuwa mitini na kwenye paa walisumbuka sana. Baadhi yetu tulisaidiwa na shirika la Msalaba Mwekundu siku kadha baadaye,” alisema mmoja wa waathiriwa Said Odha.

Akizungumza alipowatembelea waathiriwa hao Gamano, Gavana Dhadho Godhana alieleza jinsi waathiriwa hao walimpigia simu mfululizo wakiomba usaidizi.

“Nilipokea simu zenu nyingi mkisema baadhi yenu mnaishi juu kwa miti na paa za nyumba, na kwamba chakula na mifugo wenu walisombwa na maji. Tuko hapa kuhakikisha shughuli ya uokoaji inafanyika na kutathmini hasara iliyotokea,” akasema Bw Godhana.

Familia karibu 300 ziliokolewa usiku wa kuamkia Jumanne katika kijiji hicho cha Nanigi baada ya maboti 30 ya kasi kutolewa na serikali ya kaunti na kupewa shirika la Msalaba Mwekundu ili kutumika kwa operesheni hiyo.

Kulingana na Mratibu Jarred Bombe, zaidi ya asilimia 60 ya kaunti hiyo imejaa maji na kusababisha watu zaidi ya 10,000 kuhama makwao.

Wakazi wengine bado wamezingirwa na mafuriko hususan wanaoishi karibu na Mto Tana katika vijiji sita vya kaunti ndogo ya Bura.

Wanahofia kushambuliwa na mamba ambao wameonekana wakifuata maji ya mafuriko hadi vijijini.

Kwengineko, baadhi ya wakazi wa Kisii na Nyamira wamelazimika kuhama makao yao huku miundo msingi ikiharibiwa na mafuriko.

Katika soko la Kisii, wafanyibiashara walikadiria hasara kufuatia kusombwa kwa bidhaa zao za mauzo. Barabara kuu ya Kisii- Migori na ile ya Kisii- Kisumu zilifungwa kwa muda kufuatia maji yaliyosambaa barabarani.

Kamshina wa kaunti ya Kisii, Bw Godfrey Kigochi,aliwatahatharisha wakazi ambao wanaishi kando ya mto Nyakomisaro kuondoka kwa vile mto huo unazidi kufurika msimu huu wa mvua.

 

You can share this post!

Viagra huangamiza Saratani – Utafiti

Wahadhiri waapa kutumia njia zote kuendeleza mgomo wao

adminleo