• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
JAMVI: Ni pata potea kwa wafuasi wa seneta Moi huku akisalia kimya kuhusu 2022

JAMVI: Ni pata potea kwa wafuasi wa seneta Moi huku akisalia kimya kuhusu 2022

Na LEONARD ONYANGO

KIMYA kirefu cha Seneta wa Baringo, Gideon Moi, kuhusiana na ikiwa atawania urais 2022 kimewaacha wengi na maswali huku hasimu wake wa kisiasa, Naibu wa Rais William Ruto tayari akianza kampeni za mapema.

Japo kuna dalili kwamba Bw Moi atawania urais, hatajitokeza wazi kuelezea azma yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Agosti, mwaka jana.

Akizungumza katika Kanisa la Full Gospel, Kabarnet mwezi uliopita, Bw Moi aliwataka wafuasi wake kuwa na subira huku akisema atatangaza msimamo wake kuhusiana na kinyang’anyiro cha urais 2022 hivi karibuni.

Bw Moi alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na kiongozi yeyote kuhusiana na siasa za 2022.

“Wakati wa siasa haujafika lakini utakapotimia, nitawatangazia msimamo wangu. Kila mmoja ni rafiki yangu na niko tayari kufanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kubuni muungano wa kisiasa,” akasema Bw Moi.

Bw Moi alikuwa ametangaza kuwania urais katika uchaguzi uliopita lakini baadaye akabadili msimamo baada ya familia ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na baba yake, Rais Mstaafu Daniel Arap Moi.

Matokeo ya utafiti wa shirika la Ipsos yaliyotolewa mwezi uliopita yalionyesha kuwa,  Naibu wa Rais Ruto anaongoza kwa umaarufu ikilinganishwa na Bw Moi.

Utafiti huo ulionyesha kuwa, asilimia 30 ya Wakenya wanaunga mkono Bw Ruto huku asilimia 14 wakiunga Bw Moi. Utafiti huo pia ulionyesha kuwa umaarufu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye ametangaza kuwania urais na kinara wa ODM Raila Odinga ni sawa na wa Bw Moi.

Bw Moi amekuwa akiidhinishwa kuwania urais na viongozi mbalimbali kutoka Bonde la Ufa  na maeneo mengineyo ya Kenya.

Kiongozi wa hivi karibuni kuidhinisha Bw Moi ni mbunge wa Lurambi, Askofu Titus Khamala.  Mwanasiasa huyo aliyekuwa akizungumza katika eneo la Chemolingot wiki iliyopita alisema, Bw Moi ni mwana wa rais mstaafu sawa na Rais Kenyatta, hivyo hafai kushutumiwa kwa kuwania urais 2022.

Ziara ya Bw Odinga nyumbani kwa Rais Mstaafu Moi katika eneo la Kabarak pia ilifasiriwa kama mikakati ya kiongozi huyo wa upinzani kumuunga mkono, Bw Gideon Moi 2022.

Alhamisi, Bw Odinga alisema alienda kumjulia hali Rais Mstaafu baada ya kuondoka hospitalini ambapo alilazwa akitibiwa goti lake mwezi Machi.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema huenda siasa za 2022 zilikuwa ajenda kuu ya mkutano baina ya Bw Odinga na Rais Mstaafu Moi.

“Tangu Bw Odinga alipokubali kufanya kazi na Rais Kenyatta, amekuwa akikutana na viongozi ambao wanakinzana na Bw Ruto kisiasa kama vile gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo, Bw Moi kati ya wengineo.

Hiyo inaweza kufasiriwa kuwa kuna mipango inayoendelea chini kwa chini ili kumpiku Bw Ruto,” asema Bw George Mboya ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Bw Mboya, hatua ya Bw Ruto kutokutana na Bw Odinga tangu alipokubali kuunga mkono serikali ya Jubilee pia ni ishara kwamba anashuku muafaka baina ya Rais Kenyatta na kiongozi huyo wa Upinzani.

 

‘Salamu haina umaarufu’

Waandani wa Bw Ruto, wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale, walipuuzilia mbali mkutano huo baina ya Bw Odinga na Rais Mstaafu Moi wakisema hautasaidia kujipatia umaarufu kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Lakini Bw Mboya anaonya kuwa iwapo Bw Moi atachelewa kutangaza msimamo ikiwa atawania urais 2022, huenda akapata mwana si wake, haswa ikizingatiwa kwamba, tayari Bw Ruto ameanza kampeni zake za urais 2022.

Rais Kenyatta amejipata katika njiapanda ikiwa atalipa deni la Rais Mstaafu Moi aliyemuingiza katika siasa au ataunga naibu wake 2022.

Wandani wa Bw Ruto wamekuwa wakisisitiza kuwa Rais Kenyatta ndiye atakuwa kiongozi wa kampeni za naibu wake. Lakini kiongozi wa nchi amesalia kimya kuhusiana na siasa za 2022.

Bw Ruto amekuwa akikutana na viongozi kutoka maeneo mbalimbali ili kujitafutia uungwaji mkono.

Alhamisi, Bw Ruto alikutana na viongozi wa kidini kutoka eneo la Kati katika Kanisa la Anglikana mjini Kiambu. Karibu kila siku, Bw Ruto amekuwa akikutana na viongozi kutoka kaunti mbalimbali katika afisi yake mtaani Karen, Nairobi.

Bw Ruto pia amekuwa akizuru maeneo mbalimbali kama vile Kati, Magharibi na Pwani ili kujitafutia uungwaji mkono.

 

Hakuna deni

Na alipokuwa akizungumza wakati wa sherehe yake ya kurejea nyumbani tangu kuchaguliwa Agosti 8, 2017, mwanawe Rais Mstaafu Moi, Raymond Moi, alisema jamii ya Wakikuyu haina deni la Bw Ruto na haitampigia kura 2022.

Bw Raymond ambaye ni mbunge wa Rongai, Kaunti ya Nakuru, alisema nduguye Gideon ndiye atamrithi Rais Kenyatta 2022.

Alisema Mzee Moi alilipa deni la kisiasa kati ya jamii ya Wakalenjin na Wakikuyu alipomteua Rais Kenyatta kuwania urais 2002 bila mafanikio kupitia chama cha Kanu.

Bw Raymond Moi alimtaka Naibu wa Rais Bw Ruto kutotarajia kuungwa mkono na jamii ya Wakikuyu 2022.

“Nasikia baadhi ya watu wakisema kuwa jamii ya Wakikuyu inadaiwa na Wakalenjin. Hakuna deni. Mzee Jomo Kenyatta alipokuwa rais, Mzee Moi ndiye alikuwa naibu wake na alimsaidia kumwandalia uwanja kuwa rais. Mzee Moi pia alimwandaa Rais Uhuru Kenyatta kuwa rais,” akasema Bw Raymond.

 

You can share this post!

JAMVI: Mkono fiche wa mabilionea unaomtetemesha Sonko jijini

Wasiomtambua Mungu walaani mwanamke kupigwa kofi

adminleo