• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Raila atakiwa kutangaza ‘Mudavadi Tosha 2022’ kisha astaafu

Raila atakiwa kutangaza ‘Mudavadi Tosha 2022’ kisha astaafu

Na WAANDISHI WETU

BAADHI ya wabunge kutoka katika jamii ya Waluhya wanataka kinara wa Nasa Raila Odinga kustaafu siasa na kumtangaza  kinara mwenza Musalia Mudavadi kuwa mgombea urais wa muungano wa NASA kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakiongozwa na aliyekuwa seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale, wabunge hao walisema kwamba kwa mujibu wa mkataba wa Nasa wa 2017, Raila hapaswi kugombea urais mwaka wa 2022 na badala yake anafaa kumuunga mkono Bw Mudavadi.

“Mimi na maseneta James Orengo na Johnsone Muthama (aliyekuwa seneta wa Machakos) tulikuwa na wakati mgumu kuwashawishi Mudavadi na Kalonzo kutoa nafasi kwa Raila kugombea urais 2017; mkataba huo ambao ulipendekeza Mudavadi na Kalonzo kugombea urais 2022 unapaswa kuheshimiwa kwa sasa,” alisema Bw Khalwale

Akihutubu wakati wa mazishi ya mama wa mbunge wa Shinyalu Justus Kizito mwishoni mwa wiki, Bw Khalwale alisema tangu mwaka wa 2002 jamii ya Waluhya imekuwa ikimuunga mkono Raila kugombea urais na wakati umefika kwake “kurudisha mkono”.

Dkt Khalwale alisema Mudavadi alionyesha uvumlivu na ukomavu alipokubali kumwachia Raila nafasi ya kubeba bendera ya urais kupitia muungano wa Nasa 2017.

Kauli ya Khalwale iliungwa mkono na wabunge Alfred Agoi (Sabatia) Omboko Milemba (Emuhaya), Mwakilishi kutoka Kaunti ya Vihiga Beatrice Adagala, mbunge wa Lurambi Titus Khamala, mbunge wa Bumula Mwambu Mabonga na mbunge wa Mumias Mashariki Ben Washiali miongoni mwa wabunge wengine.

Wabunge hao walimlaumu Bw Odinga kwa kuwatenga vinara wenzake katika NASA kwenye muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta.

 

‘Wafuasi wana wasiwasi’

“Si tu kwamba umewasahau vinara wenzako pekee, umeaacha wafuasi wako na kiwewe,” Bw Agoi alimweleza Bw Odinga ambaye alikuwa amehudhuria mazishi ya mama wa mbunge wa eneo hilo Justus Kizito.

Bw Mabonga alimtaka Bw Odinga kustaafu siasa na kuunga mmoja wa wanasiasa wachanga.

Naye Bw Washiali alimtaka Bw Odinga kukoma kuwatumia wanasiasa wachanga kutoka jamii ya Waluhya na kisha kuwatema. Bw Mudavadi ambaye pia alihudhuria mazishi hayo, alisisitiza kuwa NASA inataka mazungumzo yanayohusisha Wakenya wote.

“Sina uhasama wa kibinafsi na Bw Odinga. Tukifotautiana, sio kwamba sisi ni maadui. Tunataka amani katika nchi hii na mazungumzo ya dhati ili watu wasije kuturuka,” alisema Bw Mudavadi.

Odinga alisisitiza kuwa anafahamu vyema mkataba wa NASA lakini akaongeza kuwa nia yake kushirikiana na Rais Kenyatta ni kuunganisha Wakenya.

“Watu wanafaa kukoma kuniita msaliti kwa sababu ya muafaka wangu na Rais Kenyatta. Siasa sio makabiliano kila wakati, kuna wakati mtu anafaa kutumia akili pia,” alisema. Alisisitiza kuwa hana nia ya kujiondoa NASA.

“Ninatafuta amani. Ni lazima turekebishe nchi yetu ambayo nusura isambaratike. Hii ndiyo sababu ninakutana na viongozi kote.

Ripoti za Titus Ominde, Benson Matheka na Shaban Makokha

You can share this post!

SHAIRI: Ziko wapi haki za wanahabari?

NMG yakanusha madai kuwa inauzwa

adminleo