• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Makamishna 3 waliojiuzulu warudishe magari ya serikali – Omtatah

Makamishna 3 waliojiuzulu warudishe magari ya serikali – Omtatah

Na SAM KIPLAGAT

MWANAHARAKATI Okiya Omtatah sasa anataka mahakama kushinikiza makamishna watatu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) waliojiuzulu warudishe magari ya serikali na walinzi.

Bw Omtatah pia anataka makamishna hao, aliyekuwa naibu wa mwenyekiti Consolata Maina, makamishna Paul Kurgat na Margaret Mwachanya wawasilishe rasmi barua za kujiuzulu.

Katika kesi yake aliyowasilisha katika Mahakama ya Leba, Bw Omtatah amesema watatu hao hawajawasilisha barua za kujiuzulu rasmi hivyo kuzuia IEBC kutangaza nafasi zao.

Alisema makamishna hao walitangaza kujiuzulu lakini hawakumkabidhi mwenyekiti wa IEBC barua za kujiuzulu kwake.

“Kutia msumari moto katika kidonda, makamishna hao bado wanaendelea kupokea mshahara, wamepewa walinzi na magari ya serikali na madereva,” anasema Bw Omtatah.

Kulingana na mwanaharakati huyo, makamishna hao wa zamani hawafai kutumia rasilimali za umma kwa sababu tayari wamejiuzulu.

“Watatu hao wanakiuka sheria kwa kuendelea kutumia rasilimali za umma licha ya wao kujiuzulu,” anasema Bw Omtatah.

Bi Maina, Bw Kurgat na Bi Mwachanya walijiuzulu wiki mbili zilizopita kutokana na kigezo kwamba hawakuwa na imani na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Anasema makamishna hao wamevunja sheria na Katiba kwa kuendelea kupata mshahara na marupurupu licha ya kujiuzulu.

You can share this post!

Rais atoa sifa kedekede kwa mwendazake Matiba

Ashangaza mpenzi kuchepuka bila haya akiiga mamake

adminleo