• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Maafisa watofautiana kuhusu kafyu ya arusi

Maafisa watofautiana kuhusu kafyu ya arusi

Na WACHIRA MWANGI

MGAWANYIKO mkubwa umeibuka kati ya maafisa wakuu wa usalama eneo la Pwani kuhusiana na marufuku ya harusi za usiku.

Haya yanajiri baada ya Kamanda wa Polisi kanda ya Pwani Noah Mwivanda kupuuzilia mbali, kama uvumi, marufuku dhidi ya harusi za usiku. Marufuku hiyo ilitangazwa na Mkuu wa Polisi kaunti ya Mombasa Johnstone Ipara.

Wiki iliyopita, Bw Ipara aliharamisha harusi za usiku akidai zinachangia visa vya makundi ya vijana kushambulia raia kwa kutumia mapanga na silaha zingine butu.

Marufuku hiyo ilitangazwa saa chache baada ya makundi hasimu ya vijana kupigana katika harusi moja. Wanachama wa makundi hayo waliweka video mitandaoni zilizoonyesha wanachama wao wakibeba mapanga wakiahidi kuendeleza shambulio. Hata hivyo, jana Bw Mwivanda alisema marufuku hiyo ni kinyume cha sheria.

“Harusi za usiku zinafaa kuendelea. Ikiwa sijapashwa habari basi, habari hizo ni uvumi tu. Amri kafyu au marufuki dhidi ya mikutano ya usiku inapasa kutoka kwangu au Mshirikishi wa Kanda Benard Leparmarai,” Bw Mwivanda akasema.

Hatua ya Bw Ipara ya kupiga marufuku harusi za kitamaduni ilipingwa na wananchi, makundi ya watetezi wa haki na wanasiasa.

Alisema makundi ya wahalifu, haswa vijana, yamekuwa yakiwalenga wanawake wanaohudhuria harusi hizo kwa nia ya kuwaibia vipuri na mali nyinginezo.

Akiwatuhubia wanahabari mjini Mombasa, Bw Mwivanda aliwataka wakazi wa Pwani kuendelea kuandaa harusi za usiku.

Hata hivyo, aliwataka kuwapasha habari maafisa wa usalama kuhusu mipango yao ya kuandaa hafla hizo ili wapewe usalama.Hii ni tofauti na amri ya Bw Ipara aliyeagiza kwamba harusi zifanyika katika kumbi za kijamii na kabla ya saa tano za usiku (11pm).

Hata hivyo, harusi nyingi za Waswahili hufanyika usiku kucha.

 

You can share this post!

Tumia muafaka kunirejesha Kenya, Miguna amlilia Raila

Maafisa 3 wa KRA wanaswa na dawa za kulevya

adminleo