• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Familia yalilia haki mwanao aliyeumwa na nyoka kufariki

Familia yalilia haki mwanao aliyeumwa na nyoka kufariki

Na KALUME KAZUNGU

FAMILIA moja kaunti ya Lamu inalilia haki baada ya mtoto wao aliyeumwa na nyoka kufariki kwa madai ya kupuuzwa hospitalini.

Philip Nyingi Murithi, 20, alifariki baada ya kuumwa na nyoka aina ya bafe akiwa shambani kwenye kijiji chao cha Sikomani. Alikuwa mwanafunzi wa shule ya upili ya Uziwa, tarafa ya Mpeketoni.

Babake mwendazake, Bw Nicholas Murithi, 60, alisema japo walimkimbiza kijana wao hospitalini mapema, madaktari na wauguzi walidai hawakuwa na dawa ya nyoka.

“Kijana wetu aliumwa na nyoka majira ya saa nne asubuhi. Tulimfikisha hospitali ya Mpeketoni mapema, lakini madaktari wakatuagiza twende hospitali kuu ya kaunti-King Fahad iliyoko mjini Lamu. Baadaye wakadai ambulensi za Mpeketoni na Witu hazingepatikana kwa wakati huo, hivyo wakaitisha ile ya Mokowe. Tulisubiri hadi saa moja usiku ndipo ambulensi ikawasili,” akasema.

Kijana alifika hospitalini saa mbili usiku hivi akiwa amelemewa na sumu ya nyoka. Walimkagua tena kabla ya kumdunga sindano. Haikuchukua muda kijana wangu akaaga,” akasema Bw Murithi.

Akijibu malalamishi hayo, Kaimu Afisa Mkuu wa Idara ya Afya Kaunti ya Lamu, Dkt David Mulewa, aliwatetea madaktari na wauguzi dhidi ya madai ya uzembe.

“Hakuna aliyezembea. Mgonjwa alidungwa sindano mbili za kumkinga dhidi ya sumu ya nyoka aliyemuuma lakini baadaye akafariki. Huenda kifo chake kinatokana na historia yake ya kimatibabu ambayo haikulingana na dawa ya nyoka aliyodungwa.

Pia kuna uwezekano mgonjwa alikaa nyumbani muda mrefu baada ya kuumwa kabla ya kufikishwa hospitalini. Huenda pia nyoka aliyemuuma ni wa sumu kali. Madaktari wetu walifanya kazi yao ipasavyo na hawastahili kulaumiwa kutokana na kifo cha kijana huyo,” akasema Dkt Mulewa.

 

You can share this post!

KFS lawamani kulemewa kuimarisha huduma za feri Mtongwe

Wakenya wengi walalamikia huduma mbovu na bei ghali ya...

adminleo