• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Leba Dei: Ni vigumu kupata ajira katika sekta rasmi

Leba Dei: Ni vigumu kupata ajira katika sekta rasmi

Na BERNARDINE MUTANU

MUUNGANO wa Waajiri nchini (FKE) umefichua kuwa kiwango cha nafasi za kazi katika sekta rasmi kimeshuka sana.

Akiongea wakati wa kuadhimisha siku ya wafanyikazi ulimwenguni Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa FKE Bi Jacqueline Mugo (pichani) alisema nafasi katika sekta rasmi zilishuka hadi asilimia 16 pekee.

Bi Mugo alisema kuna changamoto nyingi za kikazi nchini zinazohitaji kutatuliwa, “Sekta rasmi inazidi kudhoofika, kulingana na utafiti wa uchumi nchini wa hivi punde, ajira katika sekta hiyo imepungua hadi asilimia 16 pekee.”

Kiongozi huyo alisema kati ya wananchi 1.2 milioni waliohitaji kazi mwaka jana, ni 100,000 pekee waliopata kazi katika sekta rasmi, bila kujumuisha nafasi za kazi zilizotokana na uchaguzi.

“Mwaka uliopita ulikuwa mgumu sana kwetu, licha ya ushindi tuliopata, kuna changamoto kubwa zaidi,” alisema.

Katika kipindi hicho, nafasi za kazi 790,000 ziliundwa katika sekta ya jua kali, alisema, na kupendekeza kugeuzwa kwa mfumo wa ajira nchini ili kutimiza ajenda ya serikali ya maendeleo.

“Tuna ukosefu mkubwa wa ajira, inakadiriwa ni asilimia 40 nchini na wananchi wengi zaidi wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi. Kuna haja ya kugeuza sekta ya jua kali kuwa sekta rasmi iliyo na nafasi za kazi zinazoheshimika,” alisema Bi Mugo.

Mkurugenzi huyo alisema gharama kubwa ya leba nchini ilipelekea kampuni na mashirika kufuta kazi wananchi kufikia 10,000.

You can share this post!

Leba Dei: Wafanyakazi waitaka bunge kupuuza mageuzi ya...

Leba Dei: Makali ya uchumi yawatafuna zaidi Wakenya

adminleo