• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
Mvua zaidi yaja, Idara ya Utabiri yasema

Mvua zaidi yaja, Idara ya Utabiri yasema

Na WAANDISHI WETU

MVUA inatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo tofauti ya nchi wiki hii, huku mafuriko yakizidi kusababisha uharibifu.

Kulingana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa, msimu wa mvua utaendelea mwezi huu na maeneo kama vile Magharibi, Kati, Rift Valley na Pwani ndiyo yataathirika zaidi, mbali na sehemu kadhaa za Mashariki na sehemu chache Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kufuatia hali hii, Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) tawi la Mandera, kimeomba wakuu wa shule za eneo hilo na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuruhusu walimu wachelewe kurudi shuleni kwa muhula wa pili kutokana na jinsi barabara zilivyoharibiwa na mvua.

Katibu Mkuu wa chama hicho Mandera, Bw Kulow Mohamed, alisema walimu wengi wamekwama katika maeneo mbalimbali ya Kaskazini Mashariki kwa sababu ya mafuriko.

Alisema barabara zimeharibika na hazipitiki katika Kaunti za Marsabit, Garissa, Wajir na Mandera.

“Walimu wakuu na TSC wataanza kuwaadhibu walimu hawa bila kujali matatizo yanayowakumba katika msimu huu wa mvua ambao husababisha shida za usafiri,” akasema.

Katika eneo la mashariki, Serikali Kuu imeanza kusambaza chakula cha msaada kwa wakazi wa nyanda za juu za mashariki mwa Kenya, ikiwemo Kaunti za Isiolo na Marsabit, ambao nyumba zao ziliharibiwa na mafuriko.

Mratibu wa serikali katika eneo la Mashariki, Bw Wycliffe Ogallo, alisema walifanya ukaguzi kutoka angani wakatambua maeneo yaliyoathirika zaidi ni Iloret na Loiyangalani, katika kaunti hizo mbili.

Akizungumza akiwa mjini Embu, alisema mpango wa kutoa misaada utaenezwa hadi maeneo mengine yaliyoathirika.

“Tutatumia helikopta kusambaza vyakula katika maeneo hayo ili kuhakikisha hakuna atakayelala njaa,” akasema, na kuomba wanaoishi katika maeneo ambapo hukumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi wahamie maeneo salama.

Hasara iliwakumba wakazi wa eneo la Mariashoni, Elburgon wakati ng’ombe watatu na kondoo watano waliposombwa na mafuriko.

Mimea na miti pia iliharibiwa huku mvua ikizidi kunyesha katika maeneo mengi ya kaunti ndogo za Elburgon na Molo.

 

Uharibifu

Bw Samwel Kipchumba alisema mahindi yake katika ekari tatu ya shamba yaliharibiwa huku wakazi wakishangaa kwani hawajawahi kushuhudia mvua kubwa namna hiyo kwa miaka mingi.

Mvua hiyo iliyonyesha usiku wa Alhamisi pia ilitatiza usafiri katika barabara ya Elburgon kuelekea Nakuru katibu na soko la Kamwaura eneo la Njoro, baada ya bwawa la Tarakwet kuvunja kingo zake.

Usafiri kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen pia unaendelea kutatizwa na mvua kubwa ambayo imepelekea sehemu kadha za barabara hiyo kuharibika. Mnamo Jumapili, madereva na wasafiri waliokuwa kwenye msafara wa kwanza wa mabasi ya usafiri wa umma walilazimika kukaa eneo la Milihoi kwa zaidi ya saa moja baada ya daraja kwenye eneo hilo la barabara kusombwa na maji ya mafuriko.

Aidha msafara wa pili wa mabasi hayo ya usafiri wa umma haungeweza kuvuka eneo hilo, hivyo kulazimisha abiria zaidi ya 200 waliokuwa tayari wamekata tiketi kuelekea Malindi na Mombasa kukatiza safari zao.

Wasafiri wengine waliokuwa kwenye magari madogo ya kibinafsi na pikipiki wakielekea Mpeketoni na Mombasa pia walikatiza safari zao na kurudi Hindi, Mokowe na Lamu baada ya kushindwa kuvuka eneo hilo la Milihoi.

Ripoti ya VALENTINE OBARA, CHARLES WANYORO, MANASE OTSIALO, JOHN NJOROGE na KALUME KAZUNGU

You can share this post!

Niko tayari kuungana na UhuRaila kuunganisha Wakenya...

Aliyefanyiwa upasuaji vibaya akijifungua Gatundu afariki

adminleo