• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Ajenda Nne Kuu: Kijana airai serikali imkubalie azindue kiwanda cha mvinyo wa miraa

Ajenda Nne Kuu: Kijana airai serikali imkubalie azindue kiwanda cha mvinyo wa miraa

Na FAUSTINE NGILA

MARUFUKU ya Uingereza na Somaliland dhidi ya miraa kutoka Kenya iliwaacha wakulima wengi katika kaunti ya Meru katika hali duni kiuchumi, kwani ilizima njia ya kipekee ya kuzoa riziki.

Kwa wastani, mmea huo ulikuwa ukichangia Sh10 bilioni kwa pato la nchi kufikia 2013 lakini zaidi ya asilimia 75 ya pato hilo iliyeyuka baada ya marufuku hiyo iliyoanza Juni 2014.

Wakati Rais Uhuru Kenyatta aliwarai wakulima wa eneo hilo kuwekeza kwa kilimo cha mimea mbadala, wajasiriamali walianza kusaka mbinu za matumizi mapya ya miraa.

Kevin Nthiga (kulia) aelezea wateja kuhusu mvinyo, juisi, siagi na maziwa gururu (yoghurt) katika maonyesho ya teknolojia ya kilimo jijini Nairobi mwaka 2015. Picha/ Faustine Ngila

Aliyekuwa katika mstari wa mbele wa kufufua sekta ya miraa ni Kevin Nthiga ambaye wakati wa marufuku hiyo alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Ufundi na Kilimo cha Jomo Kenyatta (JKUAT), mjini Juja.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Alhamisi, kijana huyo mwenye miaka 24 alielezea jinsi alijizatiti kuanzisha kiwanda cha kutenegeneza mvinyo, sharubati, siagi na maziwa gururu (yogurt) kutokana na miraa.

“Lengo langu lilikuwa kuokoa sekta ya miraa kupitia teknolojia za kisasa. Nilibahatika kujua jinsi ya kuunda mvinyo kutokana na miraa kwenye maabara chuoni. Pia mradi wangu huo ndio ulitahiniwa na wahadhiri wangu wakati nikihitimu chuoni kwa shahada ya Sayansi ya Vyakula,” akasimulia.

Kijana Kevin Nthiga (kati) alipokutana na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Willy Bett (kushoto) na Gavana wa Meru mwaka 2017. Picha/ Faustine Ngila

Kwa muwa miraa huharibika baada ya muda mfupi, pombe na juisi inayoundwa kutokana na majani hayo inaweza kusalia dukani kwa hadi miaka miwili, kulingana naye.

“Kutengeneza mvinyo, unafaa kusaga majani mabichi ya miraa hadi upate kiwango kinachofaa cha sukari. Kisha utatia kwenye vibuyu mseto huo ili kutoa ethanol, gesi ya carbon (IV) oxide na maji. Ni ethanol hii ambayo hatimaye itatumiwa kuunda pombe,” akaelezea.

Mradi wake ulipata umaarufu mnamo 2015 na kuweza kujinasia wateja si haba katika ameneo ya Nairobi, Kiambu, Embu, Nyeri na Meru.

Mjasiriamali Kevin Nthiga aelezea vijana wenzake kuhusu teknolojia ya kuunda vinywaji kutokana na miraa. Picha/ Faustine Ngila

“Nilikuwa nikihudhuria maonyesho ya kilimo na teknolojia ili Wakenya waweze kuona na kuonja ubunifu wangu. Katika onyesho moja la shindano la miradi ya wanafunzi, nilituzwa Sh250,000 kwa kazi yangu,” akasema.

Kwenye maonyesho hayo, alikuwa akiuza bidhaa hizo kwa wateja wa kila aina walioduwazwa na mbinu iliyotumiwa kuunda bidhaa za hali ya juu kutokana na miraa.

Alikuwa anauza mvinyo kwa Sh1,000 kwa chupa ya mililita 750, maziwa gururu ya mililita 500 kwa Sh50, siagi ya robo kilo kwa Sh200 huku juisi akiiuza kwa kati ya Sh50 na Sh120.

Baadhi ya maafisa wa serikali waonja bidhaa zake. Picha/ Faustine Ngila

Kijana huyo alijiundia nembo za kuvutia kwa bidhaa zake, huku akizipakia kwenye chupa maalum ambazo marafiki zake walimsaidia kutafuta.

“Nilikuwa nimeanza kuondoa dhana potovu kuwa miraa ni mhadarati unaolevya, na ambao jamii inafaa kuepushwa nao,” akasema.

Kufikia mwishoni wa mwaka 2015, Bw Nthiga alianza kuwazia kuwekeza katika kiwanda kikubwa cha utengenezaji wa bidhaa zake hizo humu nchini, akidhamiria kupunguzia taifa hili kiwango kikubwa cha Wakenya wasio na ajira.

Kijana Nthiga alipokutana na maafisa wakuu katika Wizara ya Kilimo na kaunti ya Meru 2017. Picha/ Faustine Ngila

“Nilipohitimu JKUAT Novemba 2015, nilitazamia kusaka mbinu za kusajili kampuni yangu ya uundaji wa bidhaa ambazo tayari nilikuwa nikiuza. Nilikuwa tayari kuingia kwa mkataba na mdhamini yeyote ambaye angejitolea kunipiga jeki.”

Lakini ndoto yake hiyo hadi sasa haijatimia. Badala yake, anafundisha masomo ya kilimobiashara katika taasisi moja mjini Nyeri huku akisubiri mambo yatengee. Je, ni nini kilifanyika 2016 na 2017 na kuzima maono yake?

“Hapo 2016, nilianza kuwekeza hela nilizokuwa nmeunda. Nilinunua mashine mbili kujitayarisha kuingia kwenye soko la vinywaji. Nilinuia kusaka ufadhili wa kifedha, lakini ufadhili huo ungepatikana iwapo ningepata idhini kutoka Shirika la Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS),” anaeleza.

Juisi ya miraa iliyopakiwa kwa chupa maalum tayari kwa mauzo. Picha/ Faustine Ngila

Anasimulia kuwa alipoenda katika afisi za KEBS jijini Nairobi kuidhinishwa kuendelea na biashara yake, ilishindikana kutokana na hali kwamba KEBS haina vigezo wala mbinu za kutathmini iwapo bidhaa kutokana na miraa ni bora kwa afya ya binadamu.

Pili, uvumbuzi wake huo ulikuwa mpya sana sokoni na KEBS haikuwa imefanya utafiti kuhusu matumizi ya bidhaa za miraa awali. Ni hali hii iliyoisukuma KEBS kumtuma Bw Nthiga kwa afisi za Shirika la Kitaifa la Kupambana na Mihadarati (NACADA) ambapo pia hakupata usaidizi.

Ingawa serikali za kaunti za Embu na Meru ziliunga mkono uvumbuzi wake, mashirika hayo mawili ya serikali yalilemewa kumsaidia katika hatua muhimu za kuzindua kiwanda chake.

Juisi na mvinyo wa miraa aliokuwa akitengeneza Kevin Nthiga kwa soko la humu nchini. Picha/ Faustine Ngila

“Mwaka 2016 nilipungukiwa kabisa na hela na kukosa uwezo wa kuunda bidhaa hizo tena. Hapo ndipo nilianza kusaka ajira na kubahatika kupata kazi ya kufundisha mjini Nyeri.

“Nilikuwa nimetumia njia zote kuona teknolojia hiyo ikiwaajiri mamia ya vijana wasio na kazi. Nilifika hata kwa ofisi ya katibu wa kudumu wa Wizara ya Kilimo ambaye aliunga mkono wazo langu, lakini tatizo likasalia kuidhinishwa na KEBS na NACADA

“Mwaka 2017 nilikuatana na gavana wa Meru Kiraitu Murungi ambaye alinisikiza na kuahidi kunifadhili kupitia Shirika la Uwekezaji la Kaunti ya Meru. Kwa sasa bado ninafundisha huku nikisubiri mrejesho kutoka kwa kaunti,” akasimulia mkazi huyo wa Meru.

Kwa sasa anaiomba serikali kuu kutafuta mbinu ya kutathmini ubora wa bidhaa zake kwa kuwa ndoto yake hiyo bado inamkosesha usingizi.

Huu ndio wakati mwafaka kwa serikali kuwazia upya suala hili, has ikizingatiwa mojawapo ya Ajende Nne Kuu ni kupanua viwanda na kuunda nafasi za ajira.

Iwapo serikali itampa leseni ya kuanzisha kiwanda ambacho kitainyanyua biashara ya miraa inayotegemewa na wakulima wengi katika kaunti za Meru, Tharaka- Nithi na Embu, basi bashasha alizokuwa nazo hapo 2015 zitarejea usoni mwa kijana huyo mbunifu.

You can share this post!

RIPOTI: Ugatuzi bado unawapiga chenga vijana

Tunatambua Sossion kama kinara wa KNUT – Mahakama

adminleo