• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Mke akamatwa baada ya mwili wa mume kupatikana kwenye buti

Mke akamatwa baada ya mwili wa mume kupatikana kwenye buti

NDUNGU GACHANE na LEONARD ONYANGO

POLISI wa Mathioya, Kaunti ya Murang’a wanamhoji mke wa mwalimu wa shule ya upili ambaye maiti yake ilipatikana ikiwa imefichwa ndani ya buti ya gari Jumapili asubuhi.

OCPD wa Mathioya, Bw Charles Mutua alisema kwamba wakazi waliugundua mwili wa marehemu Samuel Mbogo, ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Gatunguru, baada ya kuona matone ya damu kutoka katika gari hilo.

“Mwili ulipatikana kwenye buti ya gari eneo la Gathukiin katika barabara ya Murang’a-Kiriaini ukiwa uchi huku macho na ulimi vikiwa vimeondolewa,” alisema Bw Mutua.

Alieleza kwamba anaamini mshukiwa Bi Alice Wachera huenda akawa na maelezo yatakayowasaidia polisi kuhusiana na kilichomuua mumewe.

“Tumeshika ili kumhoji. Huenda akatoa habari zaidi kuhusiana na tukio hili,” akasema.

Wakazi waliojawa na hofu walipata gari lililokuwa limeachwa likichuruzika damu, jambo ambalo liliwafanya kufungua mlango wa buti na ndipo walipopata maiti hiyo.

Bi Judy Njeri alisema alikuwa akienda kuuza maziwa alipokuta gari limeegeshwa kando ya barabara, kama mita 200 kutoka nyumbani kwa mwendazake.

Alisema walipata maiti ya Bw Mbogo ikiwa na majeraha usoni walipofungua gari.

Chifu wa Gathukiini Stephen Komu alisema miezi mitatu iliyopita, mwendazake aligombana na mkewe na kujeruhiwa kichwani. Mke huyo alikamatwa jana asubuhi kwa mahojiano.

Alisema gari lililokuwa likisafirisha maiti ya mwalimu mkuu lilikwama matopeni, hivyo kulazimu wauaji kutoweka huku wameliacha.

Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanaume (MAWE) Nderitu Njoka alishutumu mauaji hayo huku akiwataka polisi kuharakisha uchunguzi ili kubaini wauaji wa mwalimu huyo.

Bw Njoka alisema chama chake kimepokea malalamishi zaidi ya 50 kuhusiana na wanaume wanaotishiwa na wake wao katika Kaunti ya Murang’a.

“Vitisho hivyo pia vimeripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi lakini hatua hazijachukuliwa. Tunahimiza viongozi wa kidini humu nchini kushughulikia mizozo ya ndoa miongoni mwa waumini wao,” akasema Bw Njoka.

“Wazee wa jamii mbalimbali na viongozi wa vijiji wametelekeza jukumu lao la kuhakikisha kuwa familia zinazokumbwa na mizozo zinapatanishwa kabla ya mizozo hiyo kugeuka kuwa maafa,” akaongezea.

You can share this post!

Joho sasa aamua kushirikiana na Uhuru

Hoteli motoni kwa kuzuia mwanamke kunyonyesha

adminleo