• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Baba mkwe wa mwanamke aliyegongwa na Pasta Ng’anga asema anahofia maisha yake

Baba mkwe wa mwanamke aliyegongwa na Pasta Ng’anga asema anahofia maisha yake

Na ERIC WAINAINA

BABA MKWEWE Bi Mercy Njeri, ambaye alifariki baada ya kugongwa na gari la mhubiri James Ng’ang’a amedai kwamba maisha yake yamo hatarini.

Marehemu alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kugongwa na gari hilo katika katika Barabara Kuu ya Nairobi-Nakuru.

Jumatatu, Peter Ndung’u aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Tigoni.

Aidha, anadai kwamba kwamba watu kadhaa walivunja na kuingia nyumbani kwake katika kijiji cha Murengeti Jumapili mchana, ambapo waliingia katika vyumba vyote ila hawakuchukua chochote.

Kesi ya mauaji dhidi ya Bw Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism Centre ilitupwa wiki iliyopita na mahakama moja ya Limuru kwa msingi wa ukosefu wa ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Kulingana na Bw Mburu, watu hao waliingia kwake kwa kuvuka ua uliopo, ambapo walivunja milango yote na kuingia sebuleni.

Alisema kuwa walikaa ndani kati ya saa nne asubuhi hadi saa nane alasiri wakati yeye na familia yake walikuwa kanisani.

“Ni kama kwamba walikuwa wakitafuta kitu fulani, kwani waliingia katika kila chumba, ila hawakuchukua chochote. Hili linanaamisha kwamba hao si wezi wa kawaida,” akasema Bw Ndung’u.

Aidha, alisema kwamba aliripoti kisa hicho kwa polisi, ambapo walifika na kuandikisha taarifa kutoka kwa familia yake.

Bw Ndung’u alisema kwamba kabla ya uvamizi huo, alikuwa amegundua kwamba kuna watu kadhaa ambao walikuwa wakimfuata, hali iliyomfanya kuhofia usalama wake.

“Mapema Jumapili, nilikuwa nimefikiria kuripoti kwa polisi, kwani niliona hali hiyo kutokuwa ya kawaida. Watu wapya walikuwa wakinifuata na kunisalimia kila wakati.

Wengine wamekuwa wakiendesha pikipiki karibu na makazi yangu, hasa wakati wa usiku, jambo ambalo si la kawaida kwani nyumba yangu iko katika eneo limejificha sana,” akasema.

Na ijapokuwa alisema hana ushahidi kuhusisha matukio hayo na maamuzi ya kesi hiyo, alieleza kuwa hayo yalianza kujitokeza baada ya mahakama kutoa uamuzi huo.

Alisema kuwa hilo linapaswa kuchunguzwa mara moja.

“Hakuna hatua nyingine ningechukua, ila kuwaarifu polisi. Ningetaka wachunguze ili kubaini ikiwa hayo yana uhusiano wowote na maamuzi ya kesi hiyo,” akasema.

Kabla ya uamuzi wa kesi hiyo, familia ilikuwa imekataa juhudi za upatanisho kutoka kwa watu waliodai kutumwa na mhujbiri huyo.

 

You can share this post!

Naibu chifu alinitandika bila sababu, asema ajuza

Uchafu kwenye mazingira ulivyozidisha athari za mafuriko...

adminleo