• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Kampuni ya kupakia maji kiharamu yabambwa

Kampuni ya kupakia maji kiharamu yabambwa

Na DENNIS LUBANGA

IDARA ya Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) imegundua kiwanda haramu cha kupakia maji ya kunywa mjini Eldoret.

Maafisa wa idara hiyo mnamo Ijumaa walinasa karibu lita 1,000 za maji ya chupa katika kampuni ambayo ilikuwa ikifanya biashara hiyo bila leseni.

Kwenye mahojiano Jumapili, Meneja wa KEBS katika eneo la Rift Valley, Bw Vincent Cheruiyot, alisema kampuni ya Kalwal Holdings ilikuwa ikipakia maji ya Eldo Aqua licha ya kuwa leseni yake imepitwa na wakati.

“Tuliarifiwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa bado inaendeleza shughuli zake bila kibali. Tuliwaambia wasitishe utengenezaji bidhaa hadi wakati watakapotimiza matakwa lakini walikuwa bado wanapakia maji,” akasema Bw Cheruiyot.

Wakati wa msako, Bw Cheruiyot alisema walipata maboksi 20 yaliyokuwa na chupa 24 za maji ya lita 500 kila moja, tisa ya chupa 12 za maji ya mililita 1,000, chupa 30 za maji ya lita tano na 37 za maji ya lita 10.

Alisema kampuni hiyo ilikiuka mahitaji ya upakiaji wa maji kwenye chupa ambayo yanahitaji shughuli hiyo isifanywe katika mitaa ya makazi. Kulingana na Bw Cheruiyot, kampuni hiyo ilikuwa inafanya kazi zake katika mtaa wa Langas, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Wakati tulipozuru ghafla tulipata maji yaliyopakiwa kwenye chupa katika jengo hilo. Yalikuwa na nembo ya ubora wa bidhaa na kampuni ilikuwa ikitumia kibali cha mwaka uliopita.”

Walikuwa wamepewa muda hadi Desemba mwaka uliopita kuhamia eneo lingine nje ya mtaa wa makazi lakini hawakutimiza agizo hilo,” akasema.

Aliongeza kuwa kuna kampuni ambazo hukwepa masharti ya kisheria na hutumia ulaghai lakini akaahidi kampuni hizo zote zitapatikana na ziadhibiwe kisheria.

“Kuna kampuni ya maji ya chupa ambayo kibali chake kilipitwa na muda na sasa kinapakia maji na kusambaza kwa hospitali na hoteli. Hayo maji hayapelekwi tena madukani kwa sababu wasimamizi wa maduka ya jumla wameelimishwa na siku hizi huwa wanaitisha vibali,” akasema.

Kulingana naye, kampuni nne tayari zimepokonywa leseni kwa kutofuata masharti yanayohitajika.

  • Tags

You can share this post!

Ajali ya treni yasababisha msongamano Mombasa

DPP aahidi kunasa wafisadi wa vyeo vya juu serikalini

adminleo