• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mawaziri wahimizwa kufika bungeni kujibu maswali tata

Mawaziri wahimizwa kufika bungeni kujibu maswali tata

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amewataka mawaziri wawe wakifika bungeni kujibu maswali ya wabunge moja kwa moja.

Bw Muturi alisema hamna sheria inayowazuia mawaziri wa serikali kuu kufika bungeni kujibu maswali ambayo wabunge huuliza kwa niaba ya wananchi.

“Kwa mujibu wa kipenge 125 cha Katiba, bunge lina mamlaka ya kumwita mtu yeyote kufika mbele yake kujibu maswali, kutoa ushahidi au ufafanuzi kuhusu suala lolote lenye umuhimu kwa taifa. Ni kwa msingi ambapo mawaziri na maafisa wengine wanahitajika kufika bungeni wanapohitajika kufanya hivyo,” akasema.

Kulingana na Bw Muturi mtindo wa sasa ambapo wabunge huwasilisha majibu kwa maandishi ili yasomwe bungeni sio sawa kwani wabunge hukosa nafasi ya kuuliza maswali ya ziada ili kupata ufafanuzi zaidi.

“Huu mwenendo ambapo majibu kutoka kwa mawaziri husomwa kikasuku na wenyeviti wa kamati wasiofahamu chochote, unasinya na kuchosha. Hamna sheria inayozuia mawaziri husika kufika bungeni kujibu maswali hayo moja kwa moja na kwa ukamilifu,” Bw Muturi alisema.

Spika Muturi alitoa pendekezo hilo kwenye warsha ya maripota wa bunge katika mkahawa wa Whitesand, Mombasa.

Warsha hiyo ya siku mbili iliyokamilika Jumapili iliandaliwa na bunge la kitaifa kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari hao ( KPJA) kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuboresha ushirikiano kati ya wanahabari hao na asasi ya bunge.

Bw Muturi pia alionekana kutokubaliana na hali ya sasa ambapo mawaziri hujibu maswali katika vikao vya kamati za bunge kila Jumanne.

“Huu mtindo hauna msisimko wowote. Hii ni kwa sababu baadhi ya wenyeviti wa kamati huwakinga baadhi ya mawaziri kwa kutowapa wanachama nafasi ya kuwauliza maswali ya ziada kutokana na sababu ambazo hazieleweki,” akasema.

Alisema mfumo wa zamani ambapo kulikuwa na kipindi maalum cha maswali na majibu bunge ulifaa zaidi. Katika bunge la 11 jaribio laspika la kuwataka mawaziri kufika bungeni kujibu maswali lilipingwa na mawaziri hao kwa misingi hilo haliwezekani chini ya mfumo wa sasa wa utawala wa urais.

Walishikilia kuwa chini ya mfumo wa sasa kuna bunge na kitengo cha serikali kuu ni nguzo tofauti kwani mawaziri hawateuliwi miongoni mwa wabunge.

Bw Muturi aliwataka wanahabari kuwa macho ya umma kwa kuangazia shughuli za bunge kwa mapana na marefu.

 

You can share this post!

Mutava Musyimi: Nilinyimwa kura kwa kupinga ugawaji wa...

Jamaa apiga demu teke kwa kudoea lishe huku akimkazia asali

adminleo