• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Sakata ya NYS: Waziri Kariuki aitwa bungeni kuelezea pesa zilivyotoweka

Sakata ya NYS: Waziri Kariuki aitwa bungeni kuelezea pesa zilivyotoweka

Na LUCY KILALO

WAZIRI wa Afya ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Utumishi wa Umma, Jinsia na Vijana, Sicily Kariuki, amehitajika kufika mbele ya Kamati ya Bunge Ijumaa, kuhusiana na matumizi ya fedha katika Huduma ya Vijana ya Kitaifa(NYS).

Kamati hiyo inamtarajia kujibu masuala ibuka katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu ya 2014/15 na 2015/2016 kuhusiana na matumizi ya fedha hasa katika NYS, wakati ambapo alikuwa waziri.

“Tunachofanya ni uchunguzi wa kawaida wa ripoti za mkaguzi mkuu. Mkaguzi Mkuu bado hajatoa ripoti ya 2016/17 ambayo itashughulikia masuala ya sasa ya NYS,” mwenyekiti wa kamati hiyo, mbunge wa Ugunja, Bw Opiyo Wandayi alisema, na kuongeza kuwa kamati hiyo inaendesha wajibu wake vilivyo, tofauti na fikra kuwa haijafuata taratibu.

“Kamati inaelewa suala hilo na itafanya kazi yake bila hofu wala mapendeleo.”

Huduma hiyo ya vijana imeendelea kuandamwa na madai ya ufisadi, ya hivi punde ikiwa kashfa ya Sh9 bilioni.

Kamati hiyo pia imemtaka Waziri wa sasa, Prof Margaret Kobia kufika mbele ya kamati hiyo, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS, pamoja na wakuu wote husika wa huduma hiyo.

“Ripoti ya 2015/16 inaeleza wazi masuala yanayohusisha NYS, hasa ya bidhaa na huduma, ununuzi wa mali na bili ambazo hazijalipwa,” alisema huku akinukuu aya na kurasa za ripoti hiyo ambapo masuala hayo yamemulikwa.

Bw Wandayi alisema hayo baada ya maafisa wa wizara ya Utumishi wa Umma kukosa kufika jana kama walivyotarajiwa wakiwa wameandamana na wenzao wa mipango, hata ingawaje wizara hizo sasa ziliganywa.

Katibu wa Mipango, Dkt Julius Muia, na maafisa wake walifika, na kujitetea kuwa maswali mengi yanahusisha vitengo vingine baadhi ambavyo sasa viko chini ya wizara nyingine.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kamati ilipokea barua iliyotiwa saini na M W Ojiambo kutoka Wizara ya Utumishi wa Umma ambayo inadai kuwa hawako tayari kujibu maswali yanayotokana na ripoti hiyo ya mkaguzi mkuu.

“Kamati haijaridhishwa na sababu zilizotolewa kwa sababu ripoti hizo mbili zinazohusiana na 2014/15 na 2015/16 zilitolewa zaidi ya mwaka moja uliopita,” alisema akiongeza kuwa wanahisi kuwa kazi ya kamati hiyo imedunishwa.

 

You can share this post!

RAMADHANI: Mambo yanayoweza kuharibu saumu

MAKARIOS: Timu inayokuza vipaji vya soka mtaani Riruta

adminleo