• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Madiwani wasisitiza kupewa magari ya kifahari na pensheni

Madiwani wasisitiza kupewa magari ya kifahari na pensheni

Na VALENTINE OBARA

MADIWANI wamefufua upya wito wa kutaka wapewe pesa za kununua magari ya kifahari sawa na wabunge, na kulipwa pensheni baada ya kuhudumu kwa vipindi viwili.

Kupitia kwa Baraza la Mabunge ya Kaunti, madiwani pia wanataka kubuniwe hazina ya maendeleo ya wadi ambayo watasimamia.

Wakizungumza Jumanne kwenye mkutano wa madiwani na maseneta katika Hoteli ya Pride Inn Mombasa, maafisa wa baraza hilo walisema majukumu wanayofanya hayana tofauti kubwa na ya wabunge na hivyo wana haki ya kuinua hali yao ya maisha.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nandi, Bw Joshua Kiptoo, alisema haifai madiwani wachukuliwe kama viongozi walafi wanapopigania haki zao.

“Wakati MCA wanakutana hapa, huwa tunaambiwa tunajali tu maslahi ya wanachama wetu. Masuala tunayojadili sio ya hali ya maisha pekee.

Tunapokuja hapa kuzungumzia hali ya maisha ya wanachama wetu, kwanza tunatambua changamoto wanazopitia na kusherehekea mafanikio ya utendakazi wao,” akasema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Mabunge ya Kaunti, Bw Eric Mwangi, alisema mswada kuhusu uundaji wa hazina ya maendeleo ya wadi unafaa kupitishwa kwa kuwa madiwani ndio huwa karibu na wananchi hivyo basi wanaelewa mahitaji ya maendeleo yanayohitajika mashinani.

“Madiwani ndio wako mashinani. Wabunge wako Nairobi. Hawa ndio watu wanaotegemewa kufanikisha ugatuzi,” alisema.

You can share this post!

Waziri wa zamani ajifungia nyumbani asikamatwe na EACC

Mawimbi makali ya Jubilee, Ruto, Miguna na NASA yamgonga...

adminleo