• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
#JudiciaryForTheRich: Mahakama yashambuliwa kwa kuwanyima haki maskini

#JudiciaryForTheRich: Mahakama yashambuliwa kwa kuwanyima haki maskini

Na BENSON MATHEKA
WAKENYA Jumatano walishambulia idara ya Mahakama mtandaoni wakidai inabagua masikini na kupendelea kuamua kesi za matajiri haraka huku wasio na pesa wakiteseka.

Wakitoa maoni yao kwenye mtandao wa Twitter kufuatia ujumbe wa mwanaharakati Polycarp Hinga, Wakenya walisema mahakama zinawafunga jela masikini na kuachilia matajiri.

Bw Hinga alizua mjadala huo kwa kusema mahakama za Kenya zimetekwa na matajiri.

Waliochangia walidai  kwamba mahakama zinaharakisha kesi za matajiri huku za masikini zikichukua miaka mingi kuamuliwa.

Walitoa mfano wa wanaume watatu waliohukumiwa kufungwa jela maisha kwa kuharibu mtambo wa transfoma huku mabwenye wanaopora mabilioni wakiachiliwa huru.

“John Ndirangu, Weldon Tonui na Geoffrey Yegon walikamatwa Novemba 26 2014 katika kituo cha kibiashara cha Kahiga wakiwa na nyaya zilizoshukiwa kutoka kwa transfoma iliyoharibiwa katika shamba la Tetu, Subukia. Sote tufuatilie hii #JudiciaryForTheRich,” aliandika mmoja wa waliochangia mdahalo huo.

“Haki kwa watu matajiri inaharakishwa ilhali kwa masikini inachukua miaka mingi. Kwa mfano, kesi za mizozo ya viwandani ambazo watu masikini hutaka waajiri kuwalipa fidia ya Sh300,000 huchukua miaka mingi kuamuliwa,” alichangia Mkenya mwingine.

Mwangi X Muthiora @MwangiMuthiora  alisikitika kuwa akina mama huwa wanahangaika kortini kwa miaka wakifuatilia kesi za kubakwa kwa binti zao huku washtakiwa wakiponyoka baada ya kutumia pesa.

Baadhi ya jumbe zizowekwa kwenye mtandao wa Twitter. Picha/ Twitter

Naye  Denis Okaduyuu200F @denisokaduyu alifananisha mahakama nchini na sabuni inayoosha uhalifu kwa kuubadilisha na pesa chafu akimaanisha kuwa wahalifu hutumia pesa wanazoiba kuhakikisha wameepuka adhabu.

Akitoa hisia zake  David M. Njugunau200F @DavidMNjuguna1 alisema  watu wanaponyima haki, umasikini humea mizizi na katika hali hiyo jamii huwa inahisi kwamba kuna njama  ya kunyanyasa, kuiba na kuidunisha.

“Mahakama zetu zina mnato wa watu matajiri, sijui ni kwa nini, lakini kitu kinaniambia ni kwa sababu ya pesa na ufisadi,” alisema.

Baadhi ya waliochangia mada hiyo iliyovutia wengi walisema kwamba matajiri hupata haki kwa sababu wanaweza kuajiri mawakili shupavu kuwawakilisha  kinyume na masikini ambao baadhi hawajui umuhimu wa mawakili katika kesi.

Walisema masikini wanapoendelea kutesekea jela, matajiri huendelea kufurahia na kuwekeza pesa wanazopora kutoka kwa mali ya  umma bila kuadhibiwa.

Katika siku za hivi punde, vita dhidi ya ufisadi vimechacha huku Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji akiapa kushtaki wote wanaohusika bila kujali hadhi yao katika jamii.

You can share this post!

Starlets waanza kunoa kucha za kuiumiza Equatorial Guinea

Marufuku ya ukataji miti yaongezwa kwa miezi 6

adminleo