• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Baada ya kutemwa, kocha huyu ameshangaza kudai fidia ya Sh1 pekee!

Baada ya kutemwa, kocha huyu ameshangaza kudai fidia ya Sh1 pekee!

Na GEOFFREY ANENE

BADALA ya kupigania mabilioni baada ya kufurushwa na timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Japan, kocha Vahid Halilhodzic (pichani) ameshangaza wengi kutokana na fidia anayotaka.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Japan, mawakili wa Halilhodzic wameshtaki waajiri hao wake wa zamani Alhamisi wakitaka malipo ya yen moja ambayo ni karibu shilingi moja ya Kenya (Sh0.9) kwa “kumharibia jina na sifa.”

Raia huyu wa Bosnia & Herzegovina, ambaye ni mkazi wa Ufaransa, alitemwa kwa ghafla na Shirikisho la Soka nchini Japan (JFA) mwezi Aprili, kitendo ambacho kilikasirisha mawakili wake waliotaja njia iliyotumiwa kumfuta kazi kuwa ya “kikatili”, kinyume cha sheria.

Wakili wa Halilhodzic, Lionel Vincent amenukuliwa akisema JFA inastahili kuelezea sababu ya kupiga kalamu mteja wake na kutaka shirikisho hilo liombe msamaha.

Ameelekezea kidole cha lawama Rais wa JFA, Kozo Tashima kwa hatua ya kumtimua kocha huyu wa zamani wa Algeria, miezi miwili kabla ya Kombe la Dunia kuanza nchini Urusi, bila ya kushauriana na wanachama wa bodi.

“Kesi hii siyo ya kutafutia Vahid fedha. Alisaidia Japan kufuzu kushiriki Kombe la Dunia na hataki kudhaniwa ni mtu asiye na heshima, ambaye anaonekana mjinga. Amesikitika sana na anahisi amesalitiwa. Rais Tashima alivunja sheria ya usimamizi ya JFA kwa hivyo tunataka aombe msamaha rasmi.”

Kenya inafahamu sana hatari ya kufukuza makocha kabla ya kandarasi zao kukamilika. Mwaka 2016, Muingereza Bobby Williamson alishtaki Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika Jopo la Kuamua mizozo ya Michezo (SDT) akitaka fidia ya Sh145.9 milioni (malimbikizi ya mshahara wa miezi 12 wa Sh30 milioni, malimbikizi ya kodi ya nyumba ya miezi sita ya Sh900,000, fidia ya kuachishwa kazi ya Sh10 milioni na fidia ya miaka mitatu na nusu ya Sh105 milioni).

Mwezi Machi mwaka 2018, mzawa wa Algeria, Adel Amrouche, ambaye ni Mbelgiji, alishtaki FKF akitaka fidia ya karibu Sh132 milioni (Sh60 milioni pamoja na asilimia tano ya kiasi hiki kwa kila mwaka kutoka Machi 4, 2016 hadi kandarasi yake na Harambee Stars itakapokamilika Januari mwaka 2019).

You can share this post!

UNAI EMERY: Historia ya kocha huyu itamsaidia kuifufua...

Kamau kufika kortini baada ya wahandisi kukana kuiba...

adminleo