• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 3:55 PM
Kamau kufika kortini baada ya wahandisi kukana kuiba mamilioni

Kamau kufika kortini baada ya wahandisi kukana kuiba mamilioni

Waliokuwa wahandisi wakuu Wizara ya Uchukuzi, Mwangi Maingi (kulia) na Nicholas Ndung’u Ng’ang’a wakiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

WALIOKUWA wahandisi wakuu Wizara ya Uchukuzi walishtakiwa Jumatano huku aliyekuwa waziri, Bw Michael Kamau akiagizwa afike kortini kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka yaliyopelekea Serikali kupoteza zaidi ya Sh33 milioni miaka kumi iliyopita.

Mabw Mwangi Maingi na Nicholas Ndung’u Ng’ang’a walishtakiwa lakini Bw Kamau atafika mbele ya hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti  mnamo Mei 30 kusomewa mashtaka ya kusababisha kubadilishwa kwa ramani ya ujenzi wa barabara ya Kamukuywa-Kaptana-Kapsokwony-Sirisia mwaka wa 2008 katika kaunti ya Bungoma.

Mashtaka yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) yalisema kuwa Bw Kamau aliyekuwa ameachiliwa huru mwaka uliopita na mahakama ya rufaa kwa madai alishtakiwa wakati Tume ya kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) ilikuwa haina makamishna.

Alifikishwa kortini wakati Makamishna wa EACC wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti Bw Mumo Matemu kujiuzulu.

Naibu wa DPP Bw Alloys Kemo alimweleza Bw Ogoti kuwa maafisa wa polisi hawakumpata Bw Kamau  nyumbani kwake walipoenda kumtia nguvuni.

“Mshukiwa alikuwa ameachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na polisi waliomhoji,” alisema Bw Kemo.

Kiongozi huyo wa mashtaka aliomba korti itoe kibali cha kumtaka Bw Kamau kufika kortini kujibu mashtaka.

Bw Ogoti alikubali ombi la Bw Kemo na kumwagiza Bw Kamau afike kortini Mei 30, 2018.

Bw Kamau atashtakiwa kwa kukiuka sheria kuhusu mwongozo , usimamizi na matumizi ya pesa za umma.

Anadaiwa alifanya makosa hayo alipokuwa Katibu mkuu Wizara ya Barabara.

Bw Ogoti alitoa agizo hilo wakati waliokuwa wahandisi wawili wakuu wa Serikali Mabw  Mwangi Maingi na Nicholas Ndung’u Ng’ang’a waliposhtakiwa kwa kashfa ya kugeuza ramani ya barabara hiyo iliyokuwa imetayarishwa na kampuni ya  Enginconsult Consulting Engineers Limited.

Mahakama ilifahamishwa kubadilishwa kwa ramani hiyo kulipelekea Serikali kupoteza Sh33,303,600.

Wawili hao walidaiwa walifanya makosa hayo kati ya Oktoba 15 2007 na Machi 15 2008.

Mabw  Maingi na Ndung’u walikuwa wahandisi wakuu katika afisi za wizara ya barabara Nairobi na kaunti ya Bungoma mtawalia.

Wakili Jaji mstaafu Johnson Mitei aliwakilisha washtakiwa hao.

Aliomba waachiliwe kwa dhamana akisema polisi walikuwa wamewaachilia wawili hao kwa dhamana ya Sh100,000 na kuwataka wafike kortini jana.

“ Washtakiwa walifika kortini kama walivyoagizwa na polisi walipochukuliwa alama za vidole,” alisema Jaji Mitei.

Bw Ogoti aliwaachilia kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 na kuamuru kesi itajwe Julai 3 2018 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Baada ya kutemwa, kocha huyu ameshangaza kudai fidia ya Sh1...

Oguda amuonya Mwendwa dhidi ya safari za Harambee Stars

adminleo