• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 12:32 PM
KIBARANI: Licha ya kero lake, jaa limefaa wengi

KIBARANI: Licha ya kero lake, jaa limefaa wengi

Na CHARLES ONGADI

WIKI iliyopita, garimoshi la kubeba mafuta lilianguka eneo la Kibarani, sababu kuu ikisemekana kuwa takataka.

Unapofika Kibarani, unakaribishwa na moshi mzito unaoandamana na uvundo mkali wa takataka zilizotapakaa kila eneo mara unapoingia katika barabara ya Makupa Causeway inayounganisha Mombasa magharibi na kisiwani.

Uchafu huu na uvundo unahatarisha afya ya binadamu na viumbe vya majini vilivyoko eneo hili mbali na kutatiza hali ya mazingira na kutoa picha mbaya kwa wageni hasa watalii wanaozuru mji wa Mombasa

Jaa la Kibarani linaaminika kuwa kubwa zaidi Mombasa na kuwa tishio kwa afya, mazingira na viumbe vya majini.

Wiki chache zilizopita, Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alijipiga moyo konde na kutoa amri ya kufungwa kwa jaa hilo la tangia jadi baada ya kipindi cha miezi miwili.

“Sijui mtatumia mikakati ipi lakini nataka jaa hili la takataka lifungwe ifikapo mwezi Juni. Hamna tena kutupa takataka katika jaa hili la Kibarani,” Bw Joho alinukuliwa akisema katika vyombo vya habari.

Mchakato umeanzishwa na seriikali ya kaunti ya Mombasa kuhakikisha jaa la Kibarani linahamishwa hadi eneo la Mwakirunge (Colorado) zaidi ya kilomita 20 kutoka kitovu cha mji wa Mombasa.

Tangazo la Gavana Joho linakuja wakati wadau hasa katika sekta ya kitalii ambao wamekuwa wakilalamikia picha mbaya ambayo jaa limekuwa likitoa kwa mji wa Mombasa, unaopendwa na watalii wengi.

Ni habari zilizopokelewa kwa mikono miwili na wadau wengi Mombasa ila baadhi ikageuka kuwa hali ya huzuni na kero kuu kwao.

 

Kitega uchumi

“Jaa hili likifungwa nitaenda wapi wakati kwa muda wa miaka 35 nimekuwa hapa nikipambana na hali yangu ya kuwalea wanangu kupitia jaa hili,  , “asema Bw Nyawa Kalu mwenye umri wa miaka 67.

Bw Nyawa amekuwa akijipatia mkate wake wa kila siku kwa kuzoa mahindi, mawele, mchele na maharangwe yanayotupwa kwenye jaa hilo na kuwauzia wafanyibiashara kwa bei ya kutupa.

Anafichua kwamba alianza maisha katika jaa hilo tangu akiwa barobaro na kuishia kupata jiko na wana akiwa hapo. Anashangaa atakapowapeleka wanawe watakapofurushwa kutoka jaa hilo ambao kwao ni kama nyumbani.

Bw John Marwa Gabore , 60 , anasema kufungwa kwa jaa hilo kutawaacha zaidi ya familia 1,500 zinazoishi hapo  katika hali ya mahangaiko.

“Kazi yangu inayonilisha na kunivisha ni ya kuokota karatasi, chupa za plastiki na vyuma vikuukuu vinavyotupwa hapa kila siku na kuwauzia wafanyibiashara wanaofika na malori kuyanunua.

Nilianza kuishi na kuokota bidhaa hizi hapa mwaka wa 1982 hadi wa leo, “asema Gibore, mzaliwa wa Kuria, Kaunti ya Migori.

Bw Gibore hata hivyo anasema kwamba uamuzi wa kufungwa kwa jaa hilo haupaswi kulaumiwa bali unapaswa kuchukuliwa kama neema na baraka kwa milango mengine ya ufanisi kufunguka.

 

Watafutiwe maisha

Anamwomba Gavana Joho kuwasaidia kupata makao mengine mapya ama kuwapatia fedha za kuanzishia biashara. Mawazo ya Bw Gibore yanaungwa mkono na  mama Asha Rumba, 36, anayesema kwamba wanapaswa kupewa chochote kuanzia maisha.

‘Nimekuwa nikiokota plastiki na pia kuzoa wishwa, ngano na mahindi nakuwauzia wateja wetu, sasa itakuwaje na maisha tukifurushwa hapa?’  akauliza mama huyo wa watoto watatu.

Anasema kwamba kutokana na biashara ndogondogo anayofanya katika jaa hilo ameweza kukimu vyema watoto wake hapa bila baba yao aliyeamua kusepa mara baada ya kumzalisha.

Kwa Denis Oduori, 38,  anasema wahusika wangetafuta mbinu ya kuhakikishha kwamba wanapotoka eneo hilo wanasaidiwa kuanzisha maisha mapya akidai kwamba alikuja katika jaa hilo akiwa na wazazi wake ambao waliaga dunia miaka kadhaa iliyopita.

Kama tu wenzake, Bw Oduori amekuwa akijipatia riziki kwa kuokota chupa za plastiki na vyuma kukuu na kuwauzia wafanyibiashara.

Anasema kwamba yuko tayari kuanza maisha mapya katika jaa la Mwakirunge pindi mipango ya kuhamisha jaa hilo litakapokamilishwa.

Isack David kijana mwenye umri wa 25 anahofia kwamba endapo watafurushwa katika jaa hilo basi huenda baadhi yao wakajiunga na magenge hatari kama njia ya kujitafutia riziki.

 

Mafunzo

Anasema kwamba kabla ya kufikia hatua ya kuwaondoa eneo hilo, serikali ya kaunti ya Mombasa ingewapeleka vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa hili katika mafunzo yatakayowazesha kujipatia mkate wao wa kila siku katika siku za usoni.

David anamshukuru mfadhili mmoja kwa jina Asu aliyejitokeza na kuwajengea nyumba za mabamba na kisha kuwapeleka baadhi ya vijana katika mafunzo mbali mbali ya kujitegemea.

“Wapo Madereva, mafundi wa kupaka rangi na ujenzi na mekanika waendesha bodaboda waliofaidi kutokana na ufadhili wa Asu na ambao ingekuwa iwapo watapata mwongozo wa kupata kazi na wala siyo kuwafurusha kiholela,”asema kijana David.

Aidha, Gavana Joho amefichua kwamba serikali yake imetenga kima cha ksh 6.5 billioni kuanzisha mradi wa kugeuza takataka katika matumizi (Recycling Plant) eneo hilo la Kibarani.

Mradi huu utaweza kuwahusisha vijana na jamii katika kuhakikisha kwamba afya na mazingira  Mombasa yameweza kuthibitiwa na eneo la Kibarani kusalia kuwa safi na ya kupendeza kwa wasafiri wanaotumia barabara hiyo kuelekea uwanja wa ndege wa Moi ama makazi yao yaliyoko mitaa mbali mbali Mombasa.

 

You can share this post!

Jamii yahimizwa kukoma kuficha watu walemavu

Kisura aaibisha kakake kutangaza alifeli KCSE

adminleo