• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Ushuru yaikaribia Stima kileleni mwa jedwali Supa Ligi

Ushuru yaikaribia Stima kileleni mwa jedwali Supa Ligi

Na CECIL ODONGO

UONGOZI wa Klabu ya Western Stima katika ligi ya supa ulipunguzwa hadi alama moja baada ya wapinzani wao wakuu kwenye ligi hiyo Ushuru FC kuvuna ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya klabu ya Nakuru All Stars kwenye mechi iliyosakatwa uwanjani Camp Toyoyo siku ya Jumamosi iliyopita.

Mabao kutoka kwa wachezaji Ekaliani Ndolo, Alex Sunga na Brian Jobita iliwashuhudia watozaji ushuru hao wakimaliza mkondo wa kwanza wa ligi kwa alama 34 moja tu nyuma ya viongozi Western Stima.

Ushindani mkali hata hivyo unatarajiwa kwenye mkondo wa pili wa ligi kati ya Klabu hizo mbili ambazo awali zliteremshwa ngazi kutoka ligi ya KPL.

Hata hivyo klabu hizo zinafuatwa kwa karibu na Nairobi Stima ambao pia wametajwa kama wagombezi halisi wa ubingwa huo.

Nairobi stima pia walipata ushindi wa 3-1 dhidi ya Police FC na wanakalia nafasi ya tatu kwa alama 34 baada ya kusakata mechi zote 18 katika mkondo wa kwanza.

Wanabenki KCB waliovuna ushindi mwembamba wa 1-0 kupitia bao la mshambulizi Dennis Ngángá uwanjani Camp Toyoyo wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 33.

Ingawa Kibera Black Stars walisajili sare katika mchuano uliowakutanisha na Klabu ya St. Joseph FC wanaendelea kukwamilia nafasi ya tano kwa alama 31.

Kwa upande mwingine Klabu ya Nakuru All stars ambao wamefanya vibaya katika mkondo huo wa kwanza watahitaji miujiza ya kusajili ushindi katika mechi nyingi za mkondo wa pili ili waweze kusalia kwenye ligi hiyo.

All Stars wanaendelea kukalia eneo hatari baada ya kushinda mechi za mbili tu kati ya zote 18 za mkondo wa kwanza.

Hali hiyo hiyo inawakabili Klabu ya GFE 105 kutoka mji wa Eldoret ambao  wameshinda mechi moja tu kati ya mechi zote walizoshiriki. Kinaya ni kwamba walipata ushindi huo dhidi ya wenzao Nakuru All Stars.

You can share this post!

Sonko amnunulia mwanawe wa miaka 6 Mercedes Benz kwa...

Wakili wa Misri ataka Ramos atozwe fidia ya Sh120 bilioni...

adminleo