• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Gideon Moi apewa mwezi mmoja kugura ofisi ambayo alitengewa

Gideon Moi apewa mwezi mmoja kugura ofisi ambayo alitengewa

Na FLORAH KOECH

SENETA Gideon Moi wa Baringo amepewa mwezi mmoja kugura ofisi ambayo alitengewa katika Bunge la Kaunti hiyo.

Msajili wa Bunge hilo Joseph Koech alitoa notisi hiyo mnamo Jumanne, akisema kwamba uamuzi huo ulifanywa na Bodi ya Usimamizi wa Bunge. Bw Moi amekuwa akiendeshea shughuli zake katika ofisi hiyo tangu mwaka 2013.

Kwenye notisi hiyo, iliyoandikwa mnamo Mei 29, Bw Koech alisema kwamba afisi hiyo inapaswa kuondolewa katika bunge hilo kwa ukosefu wa nafasi ya kutosha kutokana na shughuli za ukarabati unaoendelea.

“Ninakuandikia kukueleza kuhusu uamuzi bodi ya kusimamia bunge kuondoka afisini kutokana na shughuli za ukarabati zinazoendelea. Hili pia limechangiwa na nafasi ndogo iliyopo.

Wanakandarasi wangetaka kubomoa afisi ya sasa ya Spika, ndipo tumekuandikia notisi hii,” akasema kwenye notisi hiyo.

Miezi miwili iliyopita, madiwani wanaoegemea Chama cha Jubilee (JP) walikuwa wametoa shinikizo afisi hiyo kuondolewa kwa msingi kwamba haina umuhimu wowote.

Wakiongozwa na Kiranja wa Wengi Reuben Chepsongol, walisema kwamba Bw Moi hakuwa akiitumia afisi hiyo.

“Baadhi ya kamati zetu za bunge hazina afisi, ilhali afisi ya Bw Moi haitumiki kwa shughuli zozote tangu 2013, licha ya kuwa katika bungeni. Hatuoni sababu ya kuwepo kwake, ilhali haitumiki kwa shughuli zozote,” akasema Bw Chepsongol.

Diwani Maalum Francis Kibai alisema kwamba maseneta wametengewa fedha za kukodisha afisi na Tume ya Huduma za Bunge (PSC), hivyo anapaswa kutafuta afisi kwingineko.

Hata hivyo, madiwani wa Kanu wamepinga hatua hiyo, wakidai kwamba inaendeshwa kisiasa.

Mapema 2018 kulizuka mzozo kati ya pande hizo mbili, ambapo madiwani wa Kanu waliapa kuzima juhudi zozote za kumwondoa Bw Moi katika afisi hiyo.

You can share this post!

SAKATA YA NYS: Watuhumiwa zaidi wajisalimisha kwa polisi

Buda akiri kanisani anakaranga yaya na mkewe kwa kikaango...

adminleo