• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Kiini cha Uhuru kusisimka kupiga vita ufisadi

Kiini cha Uhuru kusisimka kupiga vita ufisadi

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta ameshangaza wafuasi na wapinzani wake kwa hatua ambazo amekuwa akichukua tangu mapema mwaka huu hasa maridhiano baina yake na Raila Odinga na mwamko mpya wa kumaliza ufisadi.

Duru zinadokeza kuwa hatua hizi ni matokeo ya kutilia maanani ripoti za ujasusi na kuzitekeleza. Hii ni kinyume na awali ambapo inaaminika kuna maafisa wa ngazi za juu ambao hawakuwa makini kuhusu ripoti hizo.

Imebainika kuwa ripoti hizo za kijasusi ndizo zilizomfanya Rais Kenyatta kuridhiana na Bw Odinga. Duru zinadokeza kuwa baada ya Bw Odinga kuapishwa kuwa “rais wa wananchi” hapo Januari 31, ripoti za Idara ya Ujasusi zilimweleza Rais nchi ilikuwa katika hali mbaya, na ilikuwa vigumu kutawala iwapo Bw Odinga angeendelea na harakati zake za kupinga Serikali.

Wakati huo Bw Odinga alikuwa ameshinikiza wafuasi wake kususia bidhaa za kampuni alizodai zilisaidia katika wizi wa kura, alikuwa amejiapisha na wafuasi wake walimtambua kama rais wao, alikuwa anasukuma uchaguzi urudiwe miongoni mwa mambo mengine ambayo yalitishia kuvuruga nchi.

Duru zinasema Rais alifahamishwa na majasusi kuwa mazingira ya kisiasa yalikuwa magumu sana kwa amani, utulivu na pia utekelezaji wa ajenda yake ya maendeleo.

Rais alijulishwa kuwa katika mazingira ya Bw Odinga kuendeleza upinzani mkali dhidi ya Serikali hasa baada ya kujiapisha, nchi ingeendelea kugawanyika, shughuli za maendeleo kusimama, amani kukosekana na utawala wake ungekuwa dhaifu kiasi cha kutoweza kufanya lolote.

Ni kwa kutathmini ushauri huo ambapo Rais alishangaza wengi alipomfikia Bw Odinga kwa maridhiano kwa ajili ya nchi.

Hii ilikuwa ni moja tu ya hatua za Rais Kenyatta kufanya maamuzi kwa kutegemea ripoti za ujasusi. Nyingine ni kuwa amebadilisha mbinu yake ya kupambana na ufisadi kwa kuacha kutegemea Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na badala yake ameweka imani kwa vitengo vya ujasusi na upelelezi.

Hii ni kufuatia EACC kuonekana kulemewa na vita dhidi ya ufisadi ikizingatiwa tangu ilipobuniwa Septemba 2011 imefanya machache sana ya kujivunia katika utekelezaji wa majukumu yake. Hii imemfanya Rais Kenyatta kuonekana kama ni yeye aliyeshindwa kukabiliana na uporaji wa mali ya umma na ndiposa akaamua kubadili mbinu.

Mabadiliko haya pia yamesukumwa na haja yake ya kutimiza malengo manne makuu ya maendeleo aliyoahidi alipoapishwa kwa muhula wa pili.

Wadadisi wanasema ni ukusanyaji na utekelezaji wa habari za kijasusi ambao umefanya mambo kubadilika hasa katika kujenga uwiano na utangamano, kupigana na ufisadi na kudumisha usalama wa nchi.

 

Kusafisha idara 

Katika kuhakikisha amepiga hatua kumaliza ufisadi, Rais kwanza alisafisha idara zenye wajibu wa kufanikisha vita hivyo kwa kuwaondoa wakuu wake na kuwateua wapya.

Hii ni baada ya kubainika kuwa maafisa waliokuwa wakihudumu walikuwa wamezoea kazi kama mtindo na ilikuwa vigumu kwao kukumbatia mwamko mpya wa kupambana na ufisadi.

Wataalamu wanasema ni mabadiliko aliyofanyia kikosi cha polisi alipowaondoa maafisa wakuu punde tu baada ya kuanza kipindi chake cha pili yaliyoleta mwamko mpya. Walioondolewa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa DCI Ndegwa Muhoro, aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali Joel Kitili na mwenzake Samuel Arachi wa AP.

Katika juhudi za kufanikisha azma yake, Rais Kenyatta sasa anategemea Philip Kameru wa Huduma za Ujasusi (NIS), Joseph Boinnet (Mkuu wa Polisi), George Kinoti (Idara ya Upelelezi), Noordin Haji (Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma) na Kinuthia Mbugua (Msimamizi wa Ikulu).

Kuteuliwa kwa Bw Haji, ambaye alichukua mahala pa Keriako Tobiko kumempa Rais Kenyatta nguvu mpya za kupigana na zimwi la ufisadi ambalo lilimlemea katika kipindi chake cha kwanza.

Ushirikiano wa Bw Kameru, Boinnet, Kinoti, Haji na Mbugua umechangia mazingira ya sasa nchini. Kwenye hotuba yake ya Madaraka Dei, Rais alikiri kwamba ni kuwepo kwa maafisa wapya katika idara muhimu kunakofanikisha vita dhidi ya ufisadi.

You can share this post!

Jambazi ataka fidia ya Sh270 milioni kwa kupigwa risasi...

Walimu wachunguzwa kuhusiana na visa vya ubakaji shuleni

adminleo