• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Nyoro sasa amchoka Waititu, asema hafai

Nyoro sasa amchoka Waititu, asema hafai

Na ERIC WAINAINA

UHASAMA kati ya Gavana wa Kiambu Ferdinard Waititu na naibu wake James Nyoro hatimaye unaonekana kufikia kelele baada ya Bw Nyoro kumshutumu gavana huyo kwa uongozi mbaya.

Bw Nyoro amedai kwamba kaunti hiyo imepoteza mwelekeo kutokana na uongozi mbaya wa Gavana Waititu.

Dkt Nyoro amedai kwamba Bw Waititu amekuwa akiiendesha serikali yake bila kuzingatia sheria, hali ambayo imeifanya kupoteza ruwaza ya maendeleo waliyokuwa nayo wakati wa kampeni zao.

Uongozi wa Bw Waititu pia umewakasirisha viongozi wengine wa kaunti wakiongozwa na Seneta Kimani Wamatangi na Mwakilishi wa Wanawake, Bi Gathoni Wamuchomba.

Mnamo Jumapili, viongozi hao walikabiliana vikali na Bw Waititu baada yao kukosoa mbinu zake, hasa dhidi ya ulevi.

Walitoa mfano wa mpango wa kuwarekebisha tabia walevi, ambao unadaiwa kutumia Sh2 milioni kila siku, ila hakuna maelezo ya jinsi fedha hizo zinatumiwa.

Viongozi walidai kwamba mwelekeo ambao amechukua kukabili tatizo hilo huenda usilete manufaa ya muda mrefu.

Dkt Nyoro, aliyevunja kimya chake jana, pia alimlaumu vikali Spika wa Kaunti Stephen Ndicho na madiwani kwa “kumuunga mkono” Bw Waititu licha ya uongozi wake mbaya. Alisema hatua yao ni sawa na kuwasaliti wananchi.

Aidha, Nyoro amedai kudhulumiwa na kutengwa katika masuala muhimu yanayohusu uongozi wa kaunti.

Kwa mfano, alisema kwamba hajawahi kuhusishwa katika mikutano ya baraza la mawaziri.

Nyoro pia alidai kwamba mawaziri wamekuwa wakifanya kazi chini ya vitisho kutoka kwa Bw Waititu, akisema mtindo huo ni ukiukaji wa wazi wa Kipengele 179 cha Katiba.

“Tangu tuanze kuhudumu, hakujawahi kuwa na mkutano wa mawaziri. Ikiwa ishawahi kuwepo, basi sikuhusishwa hata kidogo. Gavana huwa anafanya maamuzi yote muhimu kibinafsi bila kumhusisha mtu yeyote. Baadhi ya maamuzi yake yanakiuka sheria. Madiwani wamekuwa wakitishwa, dhidi ya kufanya kazi nami,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa hatajiuzulu licha ya masaibu hayo.

Baadhi ya masuala aliyodai yanakiuka sheria ni uunganishaji wa kampuni za maji, hatua ya kutoipa kampuni ya Del Monte kibali kipya cha kumiliki ardhi na pendekezo la kubuni jaa la kutupia taka katika eneo la Nachu, mjini Kikuyu.

You can share this post!

Mvua kubwa yaja, Idara ya Utabiri yaonya

Zaidi ya wanasiasa 10 wagura ODM na KANU, waingia Jubilee

adminleo