• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
KIMYA CHA ‘BABA’: Raila aeleza sababu ya kutuliza boli ufisadi ukilemaza nchi

KIMYA CHA ‘BABA’: Raila aeleza sababu ya kutuliza boli ufisadi ukilemaza nchi

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amefichua sababu yake ya kupunguza presha dhidi ya serikali hata inapokumbwa na sakata za ufujaji wa mabilioni ya pesa za umma.

Wananchi wengi hasa kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakishangazwa na jinsi Bw Odinga ametulia huku ufisadi serikalini umekithiri kwani walizoea kumwona akiwa katika mstari wa mbele kukashifu serikali wakati visa kama hivyo vilipofuchuliwa katika miaka iliyotangulia.

Kwa baadhi ya wananchi, makubaliano aliyoweka na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi ulifanya upanga wake wa kukashifu makosa ya utawala wa Jubilee uwe butu kwa vile amepata majukumu serikalini yanayomletea minofu.

Hata hivyo, Bw Odinga Jumapili alisema mkwaruzano kati yake na serikali umekuwa ukiwapa washukiwa wa ufisadi nafasi ya kuingiza siasa katika juhudi za kupambana na wizi wa rasilimali ya umma, hali inayodunisha juhudi hizo kila mara.

Kupitia kwa msemaji wake Dennis Onyango, kiongozi huyo wa Chama cha ODM alisema ameamua kuachia jopokazi walilobuni pamoja na rais kutoa mapendekezo kuhusu njia bora zaidi ya kukabiliana na janga hilo.

“Muafaka wa kuleta umoja kitaifa, ambao Bw Odinga alitia sahihi, ulitambua kwamba kuingiza siasa katika vita dhidi ya wizi wa rasilimali ya umma unaotendwa na watumishi wa umma na wafanyabiashara wa kibinafsi kuliweka kizingiti kikubwa katika vita hivyo Kenya,” akasema.

Kulingana naye, washukiwa wa ufisadi walikuwa wakitumia hali hiyo kuhadaa umma kwamba hatua zinazochukuliwa dhidi yao zinalenga kuadhibu vyama vya kisiasa, jamii au viongozi mashuhuri wa kisiasa.

Bw Onyango alisema hayo kwenye taarifa aliyotoa kupuuzilia mbali ripoti kwamba Bw Odinga anaotea kuingiza wandani wake kwenye baraza la mawaziri endapo Rais Kenyatta ataamua kufanya mabadiliko ya kuondoa watumishi wa umma waliohusishwa na ufisadi.

Taarifa hiyo ilitolewa siku moja tu baada ya Bw Odinga kusitisha wito wake wa kutaka marekebisho ya katiba na kusema ameachia jopokazi walilounda na rais jukumu la kuamua kama inastahili kuwe na kura ya maamuzi.

Suala hilo lilikuwa limeanza kuibua shaka kuhusu hatima ya muafaka wa kuleta umoja wa kitaifa ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta alimuunga mkono naibu wake William Ruto na kusema hakuna haja kuwe na kura ya maamuzi wakati huu anapojitahidi kuleta maendeleo ya nchi.

Zaidi ya hayo, wabunge kadhaa wa ODM na Jubilee tayari walikuwa wameanza kulishana makucha kulihusu.

“Rais Kenyatta na Bw Odinga wameachia jopokazi la washauri masuala yote kuhusu mageuzi. Ni kundi hilo ambalo litapendekeza mwekeleo unaofaa kuchukuliwa kutatua changamoto zinazokumba nchi kwa hivyo Bw Odinga atasubiri ripoti yao.

You can share this post!

‘VIONGOZI WA KESHO’: Kaulimbiu ya UhuRuto ya...

Zabuni zinazopewa wafisadi sasa zipewe walemavu –...

adminleo