• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
Wabunge wa Zambia wazuru Kenya kufunzwa mbinu za kuzima ufisadi

Wabunge wa Zambia wazuru Kenya kufunzwa mbinu za kuzima ufisadi

Na CECIL ODONGO

KUNDI la wabunge wa Zambia linadaiwa kuwasili humu nchini kupata mafunzo maalum kuhusu njia faafu za vita dhidi ya ufisadi.

Wanachama wa Kamati ya Mamlaka na Maslahi ya Bunge la Zambia waliwatembelea makamishna wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) katika Jumba la Intergrity jijini Nairobi kujifunza kuhusu mbinu zinazotumiwa na tume hiyo kukabiliana na ufisadi.

Wabunge hao waliwasili nchini wikendi iliyopita kisha wakaandaa mkutano wao wa kwanza na makamishina wa EACC Jumatatu.

“Hii ni ziara ya kimasomo kutoka kwa wenzetu wa bunge la kitaifa la Zambia. Tunafundishana kuhusu njia za kupigana na ufisadi na uendelezaji wa maadili,” akasema kamishna wa EACC Mwaniki Gachoka.

Bi Gachoka alisema kwamba wanapigana dhidi ya ufisadi kwa kutumia mbinu tofauti mojawapo ikiwa ni uchunguzi wa kina wa kesi zinazowasilishwa na kutoa mapendekezo ya mashtaka kwa mkuu wa mashtaka ya umma(DPP).

Kiongozi wa wabunge hao Garry Nkombo alisema kwamba wanajifunza kuhusu njia kadhaa za kudhibiti ufisadi katika serikali tawala.

Bw Nkombo alisema kwamba watashauriana kuhusu mambo wanayoyapitia na matatizo wanayokumbana nayo katika kutoa taarifa za ufisadi na hukumu kwa washukiwa.

‘‘Tunatambua kwamba ufisadi upo na tunataka kujua jinsi Kenya imekuwa ikipambana nao. Tuko hapa kujua jinsi EACC imekuwa ikifanya kazi kwa kuwa ufisadi huhusisha watu mashuhuri wenye mamlaka makuu serikalini,” akasema Bw Nkombo.

Maafisa wa Kenya na mashirika ya kupigana na ufisadi yamekuwa yakiangaziwa kwa jicho la ndani baada ya kuibuka kwa sakata za ufisadi katika idara za serikali na mashirika ya umma.

Sakata ya kupotea kwa Sh9 bilioni katika Huduma ya vijana kwa taifa(NYS), Sh 1.9 kwenye Bodi ya kitaifa ya nafaka na mazao(NCPB) na Sh95 milioni katika Kampuni ya mafuta(KPC) .

Rais Uhuru Kenyatta ameonya kwamba hakuna atakayesazwa na mkono mrefu wa sheria iwapo atapatikana na hatia ya kushiriki uozo huo.

Kwa upande wake idara ya mahakama imezitaka taasisi zinazochunguza visa vya ufisadi kuwasilisha ushahidi wa kutosha ili iwe rahisi kutoa hukumu kwa wanaohusika.

You can share this post!

Minnaert afurushwa Rwanda kwa matokeo ya aibu

Wanajeshi wa Uganda wazuilia polisi wa Kenya ziwani Victoria

adminleo