• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Familia yashangaza kuandaa mazishi na harusi wakati mmoja, boma moja

Familia yashangaza kuandaa mazishi na harusi wakati mmoja, boma moja

Na STEPHEN MUTHINI

WANAKIJIJI wa Kwa Kitoo mjini Wamunyu, Kaunti ya Machakos walipigwa na butwaa baada ya familia moja kuandaa kwa pamoja hafla ya mazishi na sherehe ya harusi katika boma lao wikendi iliyopita.

Familia hiyo ilitofautiana kuhusu tarehe ya kuandaa mazishi na harusi ya mtu na dadake na kupelekea shughuli hizo kuandaliwa siku na wakati mmoja.

Deborah Wavinya Mutinda, 27, alikuwa anazikwa huku dadake mdogo Carol Syombua Mutinda, 22, naye akifanyiwa sherehe ya ndoa.

Mahema mawili yaliwekwa yakiachana kwa umbali wa mita 300 katika boma hilo la familia ya mzee Mutinda na kila kundi likaketi katika hema lake.

Ni tukio lililowashangaza wanakijiji kwani halijawahi kushuhudiwa huku wengi wakilitaja kama mwiko katika jamii ya Akamba.

Ndoa ilikuwa imepangwa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Wageni walikuwa wamefahamishwa, mahema na vyakula vikawa tayari vimenunuliwa. Chifu wa hapo Bw Justus Mutuku pia alikuwa amepokea mwaliko. Lakini msiba wa Deborah ulitokea Nairobi na kuyumbisha matayarisho ya harusi.

Wazazi wote wa familia hiyo waliaga dunia miaka miwili iliyopita, na hilo lilichangia mtafaruku uliogubika boma hilo kuhusu sherehe ipi ifanyike kwanza.

Hafla ya mazishi ya Deborah Wavinya iliyoandaliwa mita chache kutoka kwa harusi ya dadaye mdogo Carol Syombua katika kijiji cha Kwa Kitoo mjini Wamunyu, Kaunti ya Machakos. Picha/ Stephen Muthini

Kwa mujibu wa ndugu mkubwa John Mutinda ambaye sasa ndiye kiongozi wa familia, baadhi ya jamaa walitaka kuahirisha mazishi lakini jamaa wawili pamoja na kanisa ambalo Carol alikuwa akishiriki mjini Nairobi walisisitiza marehemu azikwe Jumamosi.

“Ndugu yetu Felix Mulwa na dada yetu Jackline Mwikali walisisitiza mazishi yaendelee kama ilivyopangwa,” Bw Mutinda aliambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Aliongeza: “Tulikutana kama familia kubwa chini ya uongozi wa Muoki Nzoka na kuamua hatutashiriki mazishi kwa sababu yataharibu sherehe ya ndoa.”

Bw Mutinda alisikitikia aibu iliyoipata familia yao, lakini akasema kuwa sherehe ya ndoa haingeahirishwa kwani vyakula vingeharibika pamoja na kuwa wageni wengi walikuwa njiani kuhudhuria.

Wazee kadha wa kijamii walipendekeza sherehe ya utakaso ifanywe ili kukinga familia hiyo na majanga, lakini waumini wa kanisa lililoendesha mazishi lilisitiza hakuna jambo mbaya lingetokea.

You can share this post!

Ruto akerwa na bei ghali ya mashamba jijini Nairobi

Uhuru kusherehekea Idd na Joho Mombasa

adminleo