• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
ATHARI ZA UFISADI: Wakenya wanavyoangamia kwa kuuziwa sukari yenye sumu

ATHARI ZA UFISADI: Wakenya wanavyoangamia kwa kuuziwa sukari yenye sumu

Na LEONARD ONYANGO

WAFANYABIASHARA walafi na maafisa fisadi serikalini wanachangia pakubwa katika vifo vya Wakenya kwa kuwauzia sukari yenye sumu.

Vipimo vya mahabara vilivyofanywa na Idara ya Upelelezi (DCI) vimebaini kuwa Wakenya wamekuwa wakitumia sukari iliyo na chembechembe za madini ya Mercury na shaba ambayo ni hatari kwa afya.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), madini ya mekyuri na shaba yanapoingia mwilini yanaweza kusababisha maradhi ya figo, mapafu, ubongo, kupunguza kinga za mwili na hata kusababisha kansa.

Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi nchini ya 2018 inaonyesha kuwa Wakenya wanaofariki kutokana na maradhi ya kansa inaongezeka kila mwaka, hali inayokisiwa kutokana na ulaji sumu

Mnamo 2015 watu 15,714 walifariki kutokana na kansa, watu 15,762 waliaga dunia na wengine 16,953 walikufa kwa maradhi hayo ya saratani.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i jana alisema wafanyabiashara walaghai wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA), Shirika la Kupambana na Bidhaa Ghushi (ACA) na Shirika la Kudhibiti Ubora wa Bidhaa (KEBS) kuingiza sukari na bidhaa nyingine ghushi nchini.

Waziri Matiang’i alikuwa akizungumza alipokuwa akitoa matokeo ya vipimo vya maabara vilivyofanyiwa shehena ya tani sita ya sukari ghushi iliyonaswa na polisi wiki iliyopita katika mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi na eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

“Matokeo ya vipimo vya maabara yanaonyesha kuwa sukari hii ina chembechembe za madini ya vyuma vya Mercury na shaba na ni hatari kwa afya ya binadamu,” akasema Waziri Matiang’i.

“Inahuzunisha kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakiwauzia watu sukari yenye sumu na kuua maelfu ya Wakenya,” akaongezea.

Sukari yenye sumu iliyonaswa katika eneo la Ruiru inahusishwa na mfanyabiashara mashuhuri kutoka Kaunti ya Kirinyaga, ambaye amekuwa akilindwa na wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya.

Mwanasiasa wa wa ngazi ya juu wa Jubilee kutoka Kaskazini Mashariki pia amehusishwa na sukari iliyonaswa mtaani Eastleigh.

Afisa wa Upelelezi katika idara ya DCI aliyeomba jina lake libanwe, aliambia Taifa Leo kuwa sukari hiyo yenye sumu huingizwa nchini kutoka mataifa ya kigeni, haswa Brazil, kupitia Somalia.

Sukari hiyo hupitia maeneo ya Kaskazini Mashariki na kupelekwa jijini Nairobi ambapo hupakiwa katika mifuko iliyoandikwa majina ya kampuni za sukari za Kenya.

Jumatano, Dkt Matiang’i alifichua kuwa maafisa wa polisi wanaoendesha msako wa bidhaa ghushi wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa watu ambao hakuwataja. Hiyo inamaanisha kuwa biashara hiyo inaendeshwa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

“Maafisa wetu wamekuwa wakipokea simu za vitisho. Tuko vitani na hatutarudi nyuma hata kama ni kupoteza maisha. Watu walipoteza maisha yao wakipigania uhuru wa Kenya na hata sisi hatutaogopa. Rais Kenyatta ametuagiza kukabiliana vikali na bidhaa ghushi na kazi hiyo tutafanya,” akasema Dkt Matiang’i.

Magunia ya sukari 1,365 ya kilo 50 yaliyonaswa na polisi na kuhifadhiwa katika makao makuu ya DCI yanaonyesha kuwa sukari hiyo ilitoka Brazil na Zambia.

Lakini ilipofika nchini ilipakiwa katika mifuko ya kampuni za sukari za Mumias na Nzoia.

Mifuko mingine ya sukari hiyo feki inaonyesha ilipakiwa na kampuni ya Kilimo Kenya na Transmara.

Maafisa wa polisi pia walinasa mtambo wa mabilioni ya fedha uliokuwa ukitumiwa na wafanyabiashara hao walaghai kupakia sukari katika mifuko ya kampuni za humu nchini.

You can share this post!

URUSI 2018: Fahamu vikosi vya timu zote zinazocheza fainali

Ndani miaka 105 kwa kulawiti wavulana watatu

adminleo