• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Ruto anyooshea Kalonzo mkono wa ushirikiano

Ruto anyooshea Kalonzo mkono wa ushirikiano

Na COLLINS OMULO

NAIBU RAIS William Ruto, amesema kwamba yuko tayari kushirikiana na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka ili kubadilisha siasa nchini.

Bw Ruto alisema ushirikiano mpya kati ya viongozi wa serikali na wale walio katika upinzani ni ishara tosha kwamba siasa za Kenya zimekomaa.

Kulingana na Bw Ruto, ushirikiano huo umebadilisha siasa nchini kuwa zinazojengwa kwa sera na sio zinazojikita kwa misingi ya kikabila, dini na vyama vya kisiasa.

“Sote ni Wakenya na hatutagawanywa kwa misingi ya kikabila, dini au maeneo. Msitiwe wasiwasi na wale ambao huzungumzia mikutano yetu. Watazungumza siku nzima na usiku watalala,” alisema Bw Ruto.

Alikuwa akizungumza katika hafla ya iftar iliyoandaliwa na Gavana wa Nairobi Mike Sonko mnamo Jumatano usiku katika ofisi za serikali ya jiji la Nairobi.

Akihutubu wakati wa hafla hiyo, Bw Musyoka alisema kusalimiana na kukumbatiana kunakoshuhudiwa nchini hakumaanishi kwamba upinzani umeisha makali.

Alisema wataendelea kuchunguza serikali na kwamba kushirikiana na Rais Kenyatta hakumaanishi kwamba muungano wa NASA umejiunga na Jubilee.

Kiongozi huyo wa chama cha Wiper alisisitiza kuwa wataendelea kushinikiza serikali kupigana na ufisadi akisema wizi wa pesa za umma ni uovu unaopaswa kupigwa vita na viongozi serikalini na katika upinzani.

Bw Musyoka alisema upinzani hautalegeza juhudi za kuishinikiza serikali kuangamiza ufisadi.

“Kuwa pamoja na ndugu yangu William hakumaanishi nimejiunga na Jubilee. Hata NASA kushirikiana na serikali haimaanishi serikali haitamulikwa,” alisema Bw Musyoka.

Bw Ruto alisema Kaunti ya Nairobi itakuwa ya kwanza kufaidika na nyumba za gharama ya chini katika ajenda nne kuu za serikali. Alisema mpango huo utazinduliwa katika muda wa mwezi mmoja ujao.

Alitangaza kuwa vyeti 13, 000 zaidi vya kumiliki ardhi vitatolewa jijini Nairobi baada ya 50,000 vilivyotolewa majuzi.

Bw Ruto alisema serikali itashirikiana na serikali ya Kaunti ya Nairobi kuweka lami barabara zilizo mitaa ya mabanda kuanzia mashariki mwa jiji.

“Kwa muda mrefu, Nairobi imekuwa imesahaulika lakini kwa sababu ya ushirikiano kati ya serikali ya kaunti na serikali ya kitaifa, tutabadilisha sura ya jiji ili irejelee fahari yake,” alisema.

Alimhakikishia Bw Sonko kwamba serikali ya kitaifa itaunga serikali yake.

Bw Sonko alisema kuanzia wiki ijayo, serikali yake itaanza kuajiri vijana kuzoa takataka alivyoagiza Rais Kenyatta na kwamba kuna kampuni 59 za kimataifa zinazotaka kushirikiana na serikali yake kujenga kiwanda cha kusaga taka mtaani Dandora.

You can share this post!

Joho amkaribisha Uhuru Mombasa kwa shangwe

KWAHERI UTAPIAMLO: Majani ya viazi vitamu yanavyovutia...

adminleo