• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Washukiwa wa NYS wanyimwa dhamana tena

Washukiwa wa NYS wanyimwa dhamana tena

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wote41 wa sakata mpya ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS wanaodaiwa walifuja zaidi ya Sh9 bilioni wataendelea kukaa gerezani baada ya hakimu kukataa kubatilisha masharti ya dhamana yaliyowekwa na Jaji Hedeiq Ong’undi Jumanne.

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alisema kamwe “hawezi ng’o kuvuruga amri ya Mahakama kuu licha ya tetezi washtakiwa hawawezi kulipa dhamana hiyo kwa vile wako na mapato ya viwango mbali mbali.”

Badala ya kubatilisha Bw Ogoti alitoa maagizo mapya. Jaji Ong’undi alikuwa amewaamuru washtakiwa walipe dhamana ya Sh8milioni.

Akiwaachilia kwa dhamana Jumannne , Jaji Ong’undi aliwaamuru washtakiwa walipe kila mmoja dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni , wawasilishe dhamana ya Sh5milioni na mdhamini wa Sh2milioni atakayeidhinishwa na hakimu mkuu.

Kupitia kwa mawakili wao washtakiwa wote walimlilia Bw Ogoti awabatilishie masharti waliyopewa wakisema “ itakuwa vigumu kuyatimiza.”

Akasema Bw Ogoti , “Hii mahakama haiwezi kamwe kuvuruga au kugeuza maagizo ya Jaji Ong’undi. Hii korti haina mamlaka kamwe kuingilia maamuzi ya Mahakama kuu.”

Bw Ogoti alisema kuwa jukumu ambalo Jaji huyo aliwapa mahakimu ni kuwahoji wanadhamini watakaofika kortini kuwasimamia dhamana washtakiwa.

Bw Ogoti aliwaamuru washtakiwa hao wawasilishe barua zinazoidhinisha uhalali wa hati za umiliki mashamba ama vyeti vya umiliki wa magari.

Pia aliwataka washtakiwa wawsilishe ripoti ya msajili endapo watategemea vyeti vya umiliki wa magari.

Pia aliwataka kila mmoja awasilishe kitambulisho chake cha kitaifa.

“Mbali na kitambulisho cha kitaifa kilichoidhinishwa na msajili ,,mtawasilisha hapa kortini barua iliyoandikwa na afisa anayechunguza kesi hii akihidhinisha stakabadhi zote mtakazowasilisha kama dhamana sio ghushi,” alisema Bw Ogoti.

Hakimu alisema kusikizwa kwa kesi kwapasa kung’oa nanga lakini kizingiti ni “afisi ya DPP ambayo haijawapa washtakiwa nakala za mashahidi waandae tetezi zao.”

Alitenga Julai 17 iwe siku mawakili kueleza muda watakaochukua kuwahoji mashahidi.

Mawakili zaidi ya 30 wakiongozwa na Mabw Cliff Ombeta . Kirathe Wandugi, Assa Nyakundi , Migos Ogamba na Kimani wa Wakimaa walimweleza hawajapewa nakala hizo na jitihada zao za kuzipata zimegonga mwamba.

Bw Ogoti aliamuru mmoja washtakiwa Bi Lucy Ngirita , mama ya Ann Wambere Ngirita na nduguze apelekwe kutibiwa katika hospitali kuu ya Kenyatta iwapo haridhiki na huduma anazopokea katika Kliniki cha Gereza la Langata anakozuiliwa pamoja na Katibu mkuu Wizara ya Umma , Jinsia na Vijana Bi Lillian Wanja Muthoni Mbogo Omollo.

You can share this post!

Mwanamume auawa na jeneza la mamake lililomwangukia

Mume na mke kizimbani kwa kuibia Chase Bank mamilioni

adminleo